Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 17:4-23

2 Wafalme 17:4-23 NEN

Lakini mfalme wa Ashuru akagundua kuwa Hoshea alikuwa msaliti, kwa kuwa alikuwa ametuma wajumbe kwa So mfalme wa Misri, naye hakuendelea kulipa ushuru kwa mfalme wa Ashuru tena kama alivyokuwa anafanya kila mwaka. Kwa hiyo Shalmanesa akamkamata na kumtia gerezani. Mfalme wa Ashuru akaishambulia nchi yote, akapigana dhidi ya Samaria na kuizunguka kwa majeshi miaka mitatu. Katika mwaka wa tisa wa Hoshea, mfalme wa Ashuru akaiteka Samaria na kuwahamishia Waisraeli huko Ashuru. Akawaweka huko Hala, na Gozani karibu na Mto Habori, na katika miji ya Wamedi. Yote haya yalitokea kwa sababu Waisraeli walikuwa wametenda dhambi dhidi ya BWANA Mungu wao, ambaye alikuwa amewapandisha kutoka Misri akiwatoa chini ya utawala wa nguvu wa Farao mfalme wa Misri. Waliabudu miungu mingine na kufuata desturi za mataifa ambayo BWANA alikuwa ameyafukuza mbele yao, pamoja na desturi ambazo wafalme wa Israeli walizileta. Waisraeli wakafanya vitu kwa siri dhidi ya BWANA Mungu wao, ambavyo havikuwa sawa. Kuanzia kwenye mnara wa ulinzi hadi kwenye mji wenye maboma walijijengea wenyewe mahali pa juu pa kuabudia miungu katika miji yao yote. Wakaweka mawe ya kuabudiwa na nguzo za Ashera juu ya kila kilima kirefu na chini ya kila mti uliotanda. Wakafukiza uvumba kila mahali palipoinuka, kama yalivyofanya yale mataifa ambayo BWANA alikuwa ameyafukuza mbele yao. Wakafanya mambo maovu ambayo yalimghadhibisha BWANA. Wakaabudu sanamu, ingawa BWANA alikuwa amesema, “Msifanye mambo haya.” BWANA akawaonya Israeli na Yuda kupitia kwa manabii na waonaji wake wote: “Acheni njia zenu mbaya. Shikeni amri na maagizo yangu, kufuatana na sheria yangu yote niliyowaagiza baba zenu kuitii ambayo niliileta kwenu kupitia kwa watumishi wangu manabii.” Lakini hawakusikiliza, walikuwa na shingo ngumu kama baba zao, ambao hawakumtegemea BWANA Mungu wao. Walizikataa amri zake, na agano alilokuwa amelifanya na baba zao, na maonyo aliyokuwa amewapa. Wakafuata sanamu zisizofaa, nao wenyewe wakawa hawafai. Wakayaiga mataifa yaliyowazunguka, ingawa BWANA alikuwa amewaonya akiwaambia, “Msifanye kama wanavyofanya,” nao wakafanya mambo ambayo BWANA alikuwa amewakataza wasifanye. Wakayaacha maagizo yote ya BWANA Mungu wao na kujitengenezea sanamu mbili, walizozisubu katika sura ya ndama na nguzo ya Ashera. Wakasujudia mianga yote ya angani, na wakamtumikia Baali. Wakawatoa kafara wana wao na mabinti zao katika moto. Wakafanya uaguzi na uchawi, nao wakajiuza wenyewe katika kutenda uovu machoni pa BWANA, wakamghadhibisha. Basi BWANA akawakasirikia sana Israeli na kuwaondoa kwenye uwepo wake. Ni kabila la Yuda tu lililobaki; na hata hivyo nao Yuda hawakuzishika amri za BWANA Mungu wao. Wakafuata desturi ambazo Israeli walikuwa wamezianzisha. Kwa hiyo BWANA aliwakataa watu wote wa Israeli; akawatesa na kuwaachia katika mikono ya wateka nyara hadi alipowaondoa kutoka kwenye uwepo wake. Alipokwisha kuwatenga Israeli mbali na nyumba ya Daudi, wakamfanya Yeroboamu mwana wa Nebati kuwa mfalme wao. Yeroboamu akawashawishi Israeli waache kumfuata BWANA na akawasababisha kutenda dhambi kuu. Nao Israeli wakadumu katika dhambi zote za Yeroboamu mwana wa Nebati, nao hawakuziacha hadi BWANA alipowaondoa kutoka kwenye uwepo wake, kama vile alivyokuwa ameonya kupitia watumishi wake wote manabii. Hivyo watu wa Israeli wakaondolewa kutoka nchi yao kwenda uhamishoni Ashuru, nao wako huko mpaka sasa.