Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 16:10-20

2 Wafalme 16:10-20 SRUV

Naye mfalme Ahazi akaenda Dameski ili aonane na Tiglath-pileseri mfalme wa Ashuru, akaiona ile madhabahu iliyokuwako Dameski. Mfalme Ahazi akamletea Uria kuhani namna yake ile madhabahu, na cheo chake, kama ilivyokuwa kazi yake yote. Naye Uria kuhani akajenga madhabahu; sawasawa na yote aliyomletea mfalme Ahazi kutoka Dameski; ndivyo alivyoifanya Uria kuhani iwe tayari atakaporudi mfalme Ahazi kutoka Dameski. Na mfalme aliporudi kutoka Dameski, mfalme akaiona ile madhabahu; mfalme akakaribia madhabahuni, na kutoa sadaka juu yake. Akaiteketeza sadaka yake ya kuteketezwa, na sadaka yake ya unga, akamimina sadaka yake ya kinywaji, akanyunyiza damu ya sadaka zake za amani, juu ya madhabahu. Na ile madhabahu ya shaba iliyokuwako mbele za BWANA, akaileta kutoka mbele ya nyumba, kutoka kati ya madhabahu yake mwenyewe na nyumba ya BWANA, akaiweka upande wa kaskazini wa madhabahu yake. Mfalme Ahazi akamwamuru Uria kuhani, akisema, Juu ya madhabahu hiyo kubwa uiteketeze sadaka ya kuteketezwa ya asubuhi, na sadaka ya unga ya jioni, na sadaka ya mfalme ya kuteketezwa, na sadaka yake ya unga, pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya watu wote wa nchi, na sadaka yao ya unga, na sadaka zao za kinywaji; ukanyunyize juu yake damu yote ya sadaka ya kuteketezwa, na damu yote ya dhabihu; bali madhabahu ya shaba itakuwa kwangu mimi ili niiulizie. Akafanya hivyo Uria kuhani, sawasawa na yote aliyoyaamuru mfalme Ahazi. Mfalme Ahazi akakata papi za vitako, akaliondoa lile birika juu yake; akaiteremsha ile bahari itoke juu ya ng'ombe za shaba zilizokuwa chini yake, akaiweka juu ya sakafu ya mawe. Na ukumbi wa sabato walioujenga katika hiyo nyumba, na mahali pa kuingia pake mfalme palipokuwapo nje, akavigeuza kuikabili nyumba ya BWANA, kwa sababu ya mfalme wa Ashuru. Basi mambo yote ya Ahazi yaliyosalia, aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Yuda? Ahazi akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze katika mji wa Daudi; na Hezekia mwanawe akatawala mahali pake.