Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 1:9-18

2 Wafalme 1:9-18 SRUV

Ndipo mfalme akatuma kamanda wa askari hamsini pamoja na hamsini wake, wamwendee Eliya. Akamwendea, na tazama, ameketi juu ya kilima. Akamwambia, Ewe mtu wa Mungu, mfalme asema, Shuka. Eliya akajibu, akamwambia yule kamanda wa hamsini, Ikiwa mimi ni mtu wa Mungu, na ushuke moto kutoka mbinguni, ukuteketeze wewe na hamsini wako. Moto ukashuka, ukamteketeza, yeye na hamsini wake. Akatuma tena kiongozi wa hamsini mwingine pamoja na hamsini wake, wamwendee. Akajibu, akamwambia, Ewe mtu wa Mungu, mfalme asema, Shuka upesi. Eliya akajibu, akamwambia, Ikiwa mimi ni mtu wa Mungu, na ushuke moto kutoka mbinguni, ukuteketeze wewe na hamsini wako. Moto wa Mungu ukashuka kutoka mbinguni, ukamteketeza, yeye na hamsini wake. Tena akatuma kamanda wa hamsini wa tatu, pamoja na hamsini wake. Yule kamanda wa hamsini wa tatu akapanda, akaenda akapiga magoti mbele ya Eliya, akamsihi sana, akamwambia, Ee mtu wa Mungu, nakusihi, roho yangu, na roho za watumishi wako hawa hamsini, ziwe na thamani machoni pako. Tazama, moto ulishuka kutoka mbinguni, ukawateketeza wale kamanda wa hamsini wawili wa kwanza pamoja na hamsini wao; laiti sasa roho yangu na iwe na thamani machoni pako. Malaika wa BWANA akamwambia Eliya, Shuka pamoja naye; usimwogope. Akaondoka, akashuka pamoja naye hadi kwa mfalme. Akamwambia, BWANA asema hivi, Kwa kuwa umetuma wajumbe waulize kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni, je! Ni kwa sababu hakuna Mungu katika Israeli, uulize neno lake? Kwa hiyo hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa. Basi akafa, sawasawa na neno la BWANA alilolinena Eliya. Na Yoramu alianza kutawala mahali pake katika mwaka wa pili wa Yehoramu mwana wa Yehoshafati mfalme wa Yuda; kwa kuwa yeye hakuwa na mwana. Na mambo yote yaliyosalia aliyoyafanya Ahazia, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Israeli?