Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samweli 28:15-25

1 Samweli 28:15-25 SRUV

Ndipo Samweli akamwambia Sauli, Mbona umenitaabisha mimi, hata kunipandisha juu? Sauli akajibu, Mimi nimetaabika sana; kwa kuwa hao Wafilisti wananifanyia vita, naye Mungu ameniacha; hanijibu tena, wala kwa manabii, wala kwa ndoto; kwa hiyo nimekuita wewe, ili wewe unijulishe nifanyeje. Samweli akasema, Kwa nini unaniuliza mimi, wakati BWANA amekuacha, naye amekuwa adui yako? Yeye BWANA amekutendea kama alivyosema kwa kinywa changu; BWANA amekurarulia ufalme mkononi mwako, na kumpa jirani yako, yaani, Daudi. Kwa sababu wewe hukuitii sauti ya BWANA, wala hukumtimilizia hasira yake kali juu ya Amaleki; kwa sababu hii BWANA amekutendea hili leo. Tena pamoja na wewe BWANA atawatia Israeli mikononi mwa Wafilisti; hata na kesho wewe na wanao mtakuwapo pamoja nami; tena BWANA atawatia jeshi la Israeli pia mikononi mwa Wafilisti. Mara Sauli akaanguka chini kifudifudi, akaingiwa na hofu kuu kwa sababu ya maneno hayo ya Samweli, wala hakuwa na nguvu yoyote; kwa maana hakula chakula mchana kutwa, wala usiku kucha. Ndipo yule mwanamke akamwendea Sauli na alipoona kuwa yeye ametaabika sana, akamwambia, Angalia, mjakazi wako ameisikiliza sauti yako, nami nimehatarisha uhai wangu, nami nimeyasikiliza maneno yako uliyoniambia. Basi sasa, tafadhali, wewe uisikilize sauti ya mjakazi wako, nikakuandalie angaa mkate kidogo; ukale, ili upate nguvu, utakapokwenda zako. Lakini yeye alikataa, akasema, Mimi sitaki kula. Ila watumishi wake, pamoja na yule mwanamke, wakamlazimisha; naye akaisikiliza sauti yao. Basi akainuka hapo chini, akaketi juu ya kitanda. Naye yule mwanamke alikuwa na ndama aliyenona nyumbani; akafanya haraka kumchinja; akatwaa na unga, akaukanda, akafanya mkate wa mofa kwa unga huo; kisha akamwandalia Sauli na watumishi wake; wakala. Ndipo wakaondoka, wakaenda zao usiku ule.