1 Samweli 2:25-35
1 Samweli 2:25-35 SRUV
Mtu mmoja akimkosea mwenzake, Mungu atamhukumu; lakini mtu akimkosea BWANA, ni nani atakayemtetea? Lakini hawakuisikia sauti ya baba yao, kwa sababu BWANA amekusudia kuwaua. Na yule mtoto, Samweli, akazidi kukua akapata kibali kwa BWANA, na kwa watu pia. Kisha mtu wa Mungu akamwendea Eli, akamwambia, BWANA asema hivi, Je! Mimi sikujidhihirisha nafsi yangu kwa nyumba ya baba yako, walipokuwa katika Misri, wakiitumikia nyumba ya Farao? Je! Sikumchagua yeye katika kabila zote za Israeli, ili awe kuhani wangu, apande madhabahuni kwangu; na kufukiza uvumba, na kuvaa naivera mbele zangu? Nami sikuwapa watu wa koo za baba yako dhabihu zote za wana wa Israeli zilizotolewa kwa moto? Kwa nini basi mnaipiga teke dhabihu yangu na sadaka yangu nilizoziamuru katika maskani yangu; ukawaheshimu wanao kuliko mimi, mpate kujinenepesha kwa sadaka zote za watu wangu Israeli zilizo njema? Kwa sababu hiyo, BWANA, Mungu wa Israeli, asema, Ni kweli, nilisema ya kuwa nyumba yako, na nyumba ya baba yako itakwenda mbele zangu milele; lakini sasa BWANA asema, Jambo hili na liwe mbali nami; kwa maana wao wanaoniheshimu nitawaheshimu, na wao wanaonidharau nitawadharau. Angalia, siku zinakuja, nitakapoukata mkono wako, na mkono wa watu wa ukoo wa baba yako, hata nyumbani mwako hapatakuwako mzee. Nawe utayatazama mateso ya maskani yangu, katika utajiri wote watakaopewa Israeli; wala nyumbani mwako hapatakuwako mzee milele. Tena mtu wako, ambaye sitamtenga na madhabahu yangu, atakuwa mtu wa kukupofusha macho, na kukuhuzunisha moyo; tena wazao wote wa nyumba yako watakufa watakapokuwa watu wazima. Na yatakayowapata wana wako wawili, Hofni na Finehasi; ndiyo ishara itakayokuwa kwako; wote wawili watakufa siku moja. Nami nitajiinulia kuhani mwaminifu, atakayefanya kulingana na yale yaliyo katika moyo wangu na katika akili yangu; nami nitamjengea nyumba iliyo imara; naye atakwenda mbele ya masihi wangu milele.