1 Samweli 2:25-35
1 Samweli 2:25-35 NEN
Kama mtu akifanya dhambi dhidi ya mtu mwenzake, mtu mwingine aweza kumwombea kwa Mungu, lakini kama mtu akimfanyia Mungu dhambi, ni nani atakayemwombea?” Hata hivyo wanawe hawakusikia maonyo ya baba yao, kwa sababu BWANA alitaka kuwaua. Naye kijana Samweli akaendelea kukua katika kimo, akimpendeza BWANA na wanadamu. Basi mtu wa Mungu akaja kwa Eli na kumwambia, “Hivi ndivyo asemavyo BWANA: ‘Je, sikujifunua waziwazi kwa nyumba ya baba yako wakati walikuwa huko Misri chini ya Farao? Nilimchagua baba yako kati ya makabila yote ya Israeli kuwa kuhani wangu, kukwea kwenye madhabahu yangu, kufukiza uvumba na kuvaa kisibau mbele yangu. Pia niliwapa nyumba ya baba yako sadaka zote zilizotolewa kwa moto na Waisraeli. Kwa nini unadharau dhabihu zangu na sadaka zile nilizoziamuru kwa ajili ya makao yangu? Kwa nini unawaheshimu wanao kuliko mimi kwa kujinenepesha wenyewe kwa kula sehemu zilizo bora za kila sadaka zinazotolewa na watu wangu wa Israeli?’ “Kwa hiyo, BWANA, Mungu wa Israeli asema: ‘Niliahidi kuwa nyumba yako na nyumba ya baba yako wangehudumu mbele zangu milele.’ Lakini sasa BWANA anasema: ‘Jambo hili na liwe mbali nami! Wale wanaoniheshimu nitawaheshimu, wale wanaonidharau mimi watadharauliwa. Wakati unakuja nitakapozipunguza nguvu zenu na nguvu ya nyumba ya baba yenu, ili pasiwepo mtu katika mbari yenu atakayeishi kuuona uzee nanyi mtaona huzuni katika makao yangu. Ingawa Israeli watafanyiwa mema, katika mbari yenu kamwe hapatakuwepo mtu atakayeishi hadi kuwa mzee. Kila mmoja wenu ambaye sitamkatilia mbali kutoka madhabahuni pangu atabakizwa tu kupofusha macho yenu kwa machozi na kuihuzunisha mioyo yenu, nao wazao wenu wote watakufa watakapokuwa wamefikia umri wa kustawi. “ ‘Kile kitakachotokea kwa wanao wawili, Hofni na Finehasi, kitakuwa ishara kwako. Wote wawili watakufa katika siku moja. Mimi mwenyewe nitajiinulia kuhani mwaminifu, ambaye atafanya sawasawa na kile kilichoko moyoni mwangu na akilini mwangu. Nitaifanya nyumba yake kuwa imara, naye atahudumu mbele ya mpakwa mafuta wangu daima.