Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samweli 16:1-12

1 Samweli 16:1-12 SRUV

BWANA akamwambia Samweli, utamlilia Sauli hadi lini, kwa kuwa mimi nimemkataa asiwatawale Waisraeli? Ijaze pembe yako mafuta, uende, nami nitakutuma kwa Yese, Mbethlehemi; maana nimejipatia mfalme katika wanawe. Samweli akasema, Nawezaje kwenda? Sauli akipata habari, ataniua. Basi BWANA akasema, Chukua ndama pamoja nawe, ukaseme, Nimekuja ili kumtolea BWANA dhabihu. Umwalike Yese aje kwenye dhabihu, nami nitakuonesha utakayotenda; nawe utampaka mafuta yule nitakayemtaja kwako. Samweli akafanya hayo aliyosema BWANA, akaenda Bethlehemu. Wakaja wazee wa mji kumlaki, wakitetemeka, nao wakasema, Je! Umekuja kwa amani? Naye akasema, Naam, kwa amani; nimekuja kumtolea BWANA dhabihu; jitakaseni; njoni pamoja nami kwenye dhabihu. Akawatakasa Yese na wanawe, akawaita kwenye dhabihu. Ikawa walipokuja, alimtazama Eliabu, akasema, Yakini masihi wa BWANA yupo hapa mbele zake. Lakini BWANA akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. BWANA haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali BWANA huutazama moyo. Ndipo Yese akamwita Abinadabu, akampitisha mbele ya Samweli. Naye akasema, BWANA hakumchagua huyu. Ndipo Yese akampitisha Shama. Naye akasema, Wala BWANA hakumchagua huyu. Yese akawapitisha wanawe saba mbele ya Samweli. Samweli akamwambia Yese, BWANA hakuwachagua hawa. Kisha Samweli akamwambia Yese, Watoto wako wote wapo hapa? Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama, anawachunga kondoo. Basi Samweli akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa sababu hatutaketi hadi atakapokuja huku. Basi akatuma mtu, naye akamleta kwao. Naye alikuwa mwekundu, mwenye macho mazuri, na umbo lake lilikuwa la kupendeza. BWANA akasema, Ondoka, umtie mafuta; maana huyu ndiye.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 1 Samweli 16:1-12