Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samweli 1:1-11

1 Samweli 1:1-11 SRUV

Palikuwa na mtu mmoja wa Rama, Msufi, wa nchi ya milima milima ya Efraimu, jina lake akiitwa Elkana, mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu, mwana wa Tohu, mwana wa Sufu, Mwefraimu naye alikuwa na wake wawili; jina lake mmoja akiitwa Hana, na jina lake wa pili aliitwa Penina; naye huyo Penina alikuwa na watoto, lakini Hana hakuwa na watoto. Na mtu huyo alikuwa akikwea kutoka mjini kwake mwaka kwa mwaka, ili kuabudu, na kumtolea BWANA wa majeshi dhabihu katika Shilo. Na wale wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, makuhani wa BWANA, walikuwako huko. Hata siku ile ilipofika Elkana alipotoa dhabihu, kumpa mkewe Penina sehemu, akawapa na watoto wake wote, wanaume kwa wanawake, sehemu zao; lakini Hana humpa sehemu mara mbili; maana alimpenda Hana, ingawa BWANA alikuwa amemfunga tumbo. Ila mwenzake humchokoza sana, ili kumwuudhi, kwa sababu BWANA alikuwa amemfunga tumbo. Tena mumewe akafanya hivyo mwaka kwa mwaka, hapo yule mwanamke alipokwea kwenda nyumbani kwa BWANA, ndivyo yule alivyomchokoza; basi, kwa hiyo, yeye akalia, asile chakula. Elkana mumewe akamwambia, Hana, unalilia nini? Kwa nini huli? Kwa nini moyo wako una huzuni? Je! Mimi si bora kwako kuliko watoto kumi? Ndipo Hana akainuka, walipokula na kunywa huko Shilo. Naye Eli, kuhani, alikuwa akiketi kitini pake penye mwimo wa hekalu la BWANA. Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba BWANA akalia sana. Akaweka nadhiri, akasema, Ee BWANA wa majeshi, ikiwa wewe utayaangalia mateso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto wa kiume, ndipo mimi nitakapompa BWANA huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikia kichwani kamwe.