1 Wafalme 8:22-30
1 Wafalme 8:22-30 SRUV
Sulemani akasimama mbele ya madhabahu ya BWANA, machoni pa mkutano wote wa Israeli, akaikunjua mikono yake mbinguni. Akasema Ee BWANA, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe, mbinguni juu wala duniani chini; ushikaye maagano na rehema kwa watumishi wako, waendao mbele zako kwa mioyo yao yote. Umemtimizia mtumishi wako, Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidia; naam, ulinena kwa kinywa chako, ukayatimiza kwa mkono wako, kama ilivyo leo. Na sasa, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, umtimizie mtumishi wako, Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidia, ukisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli machoni pangu, kama watoto wako wakiangalia njia zao, ili kuenenda mbele zangu kama wewe ulivyoenenda. Sasa, Ee Mungu wa Israeli, nakusihi, ulithibitishe neno lako, ulilomwambia mtumishi wako, Daudi, baba yangu. Lakini Mungu je? Hakika atakaa juu ya nchi? Tazama, mbingu hazikutoshi, wala mbingu za mbingu; sembuse nyumba hii niliyoijenga! Lakini uyaelekee maombi ya mtumwa wako, na dua yake, Ee BWANA, Mungu wangu, uisikilize sauti na maombi ya mtumwa wako, aombayo mbele zako leo. Macho yako yafumbuke na kuielekea nyumba hii usiku na mchana, mahali hapa ulipopataja, ukasema, Hapa ndipo litakapokuwapo jina langu; ili uyasikie maombi ya mtumwa wako aombapo akikabili mahali hapa. Uisikie dua ya mtumwa wako, na ya watu wako Israeli, watakapoomba wakikabili mahali hapa; naam, sikia huko mbinguni, makao yako; nawe usikiapo, samehe.