1 Wafalme 8:1-11
1 Wafalme 8:1-11 SRUV
Ndipo Sulemani alipowakusanya wazee wa Israeli, na wakuu wote wa makabila na wakuu wa koo za wana wa Israeli, wamwendee mfalme Sulemani huko Yerusalemu, ili walipandishe sanduku la Agano la BWANA kutoka mji wa Daudi, yaani, Sayuni. Watu wote wa Israeli wakakutana mbele ya mfalme Sulemani wakati wa sikukuu, katika mwezi wa Ethanimu, ndio mwezi wa saba. Wazee wote wa Israeli wakaja, nao makuhani wakajitwika sanduku. Wakalipandisha sanduku la BWANA, na ile hema ya kukutania, na vyombo vitakatifu vyote vilivyokuwa katika ile Hema; vitu hivyo makuhani na Walawi wakavipandisha. Mfalme Sulemani, na mkutano wote wa Israeli waliokutanika kwake, walikuwako pamoja naye mbele ya sanduku, wakichinja sadaka kondoo na ng'ombe, wasioweza kuhesabiwa wala idadi yao kujulikana kwa kuwa wengi. Makuhani wakalileta sanduku la Agano la BWANA hadi mahali pake, katika chumba cha ndani cha ile nyumba, patakatifu pa patakatifu, naam, chini ya mbawa za makerubi. Kwa maana makerubi yalinyosha mbawa zao, juu ya mahali pa sanduku, makerubi yakalifunika lile sanduku na miti yake kwa juu. Na ile miti kwa kuwa mirefu, ncha za miti zilionekana katika mahali patakatifu, mbele ya chumba cha ndani; lakini hazikuonekana nje; nayo iko kuko huko hata leo. Hamkuwa na kitu ndani ya sanduku, ila zile mbao mbili za mawe ambazo Musa aliziweka ndani huko Horebu, BWANA alipofanya agano na wana wa Israeli, hapo walipotoka katika nchi ya Misri. Ikawa, makuhani walipotoka katika patakatifu, nyumba ya BWANA ikajaa wingu; hata makuhani hawakuweza kusimama ili kufanya huduma yao, kwa sababu ya wingu lile; kwa kuwa nyumba ya BWANA ilikuwa imejaa utukufu wa BWANA.