Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 8:1-11

1 Wafalme 8:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ndipo Sulemani alipowakusanya wazee wa Israeli, na wakuu wote wa kabila, wakuu wa mbari za mababa wa wana wa Israeli, wamwendee mfalme Sulemani huko Yerusalemu, ili walipandishe sanduku la agano la BWANA kutoka mji wa Daudi, yaani, Sayuni. Wakakutana mbele ya mfalme Sulemani watu wote wa Israeli wakati wa sikukuu, katika mwezi wa Ethanimu, ndio mwezi wa saba. Wazee wote wa Israeli wakaja, nao makuhani wakajitwika sanduku. Wakalipandisha sanduku la BWANA, na ile hema ya kukutania, na vyombo vitakatifu vyote vilivyokuwa katika ile Hema; vitu hivyo makuhani na Walawi wakavipandisha. Mfalme Sulemani, na mkutano wote wa Israeli waliokutanika kwake, walikuwako pamoja naye mbele ya sanduku, wakichinja sadaka kondoo na ng’ombe, wasioweza kuhesabiwa wala kufahamiwa idadi yao kwa kuwa wengi. Makuhani wakalileta sanduku la agano la BWANA hata mahali pake, katika chumba cha ndani cha ile nyumba, patakatifu pa patakatifu, naam, chini ya mbawa za makerubi. Kwa maana makerubi yalinyosha mbawa zao, juu ya mahali pa sanduku, makerubi yakalifunika lile sanduku na miti yake kwa juu. Na ile miti kwa kuwa mirefu, ncha za miti zilionekana katika mahali patakatifu, mbele ya chumba cha ndani; lakini hazikuonekana nje; nayo iko kuko huko hata leo. Hamkuwa na kitu ndani ya sanduku, ila zile mbao mbili za mawe ambazo Musa aliziweka ndani huko Horebu, BWANA alipofanya agano na wana wa Israeli, hapo walipotoka katika nchi ya Misri. Ikawa, makuhani walipotoka katika patakatifu, nyumba ya BWANA ikajaa wingu; hata makuhani hawakuweza kusimama ili kufanya huduma yao, kwa sababu ya wingu lile; kwa kuwa nyumba ya BWANA ilikuwa imejaa utukufu wa BWANA.

1 Wafalme 8:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

Basi, mfalme Solomoni akawakutanisha mbele yake huko Yerusalemu wazee na viongozi wote wa makabila na wa koo za Israeli ili waliondoe sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu katika mji wa Daudi, yaani Siyoni. Wakati wa sikukuu ya mwezi wa Ethanimu, yaani mwezi wa saba. Ndipo watu hao wote walipokusanyika mbele ya mfalme Solomoni. Baada ya wazee wote wa Israeli kuwasili, makuhani walibeba sanduku la agano. Walawi na makuhani walihamisha sanduku la agano na hema la mkutano, na vyombo vitakatifu vyote vilivyokuwa humo hemani. Mfalme Solomoni na mkutano wote wa Israeli wakakusanyika mbele ya sanduku la agano, nao wakatoa tambiko: Ng'ombe na kondoo wasiohesabika. Kisha makuhani wakaliingiza sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu mahali pake, katika chumba cha ndani cha nyumba mahali patakatifu sana, chini ya mabawa ya viumbe wenye mabawa. Hao viumbe wenye mabawa walitandaza mabawa yao juu ya mahali lilipowekwa sanduku, kwa hiyo sanduku na mipiko yake ya kulibebea vilikuwa chini ya mabawa. Kwa kuwa mipiko hiyo ilikuwa mirefu sana, ncha zake ziliweza kuonekana kutoka mahali patakatifu, mbele ya chumba cha ndani; lakini haikuweza kuonekana kutoka upande wa nje. Mipiko hiyo ingali mahali hapo hata leo. Hapakuwa na kitu ndani ya sanduku la agano ila vile vibao viwili vya mawe ambavyo Mose aliviweka humo kule Horebu, mahali Mwenyezi-Mungu alipofanya agano na Waisraeli walipotoka nchini Misri. Ikawa, makuhani walipotoka pale mahali patakatifu, wingu liliijaza nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Nao makuhani walishindwa kuhudumu kwa sababu ya wingu hilo; kwa kuwa utukufu wa Mwenyezi-Mungu uliijaza nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

1 Wafalme 8:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ndipo Sulemani alipowakusanya wazee wa Israeli, na wakuu wote wa makabila na wakuu wa koo za wana wa Israeli, wamwendee mfalme Sulemani huko Yerusalemu, ili walipandishe sanduku la Agano la BWANA kutoka mji wa Daudi, yaani, Sayuni. Watu wote wa Israeli wakakutana mbele ya mfalme Sulemani wakati wa sikukuu, katika mwezi wa Ethanimu, ndio mwezi wa saba. Wazee wote wa Israeli wakaja, nao makuhani wakajitwika sanduku. Wakalipandisha sanduku la BWANA, na ile hema ya kukutania, na vyombo vitakatifu vyote vilivyokuwa katika ile Hema; vitu hivyo makuhani na Walawi wakavipandisha. Mfalme Sulemani, na mkutano wote wa Israeli waliokutanika kwake, walikuwako pamoja naye mbele ya sanduku, wakichinja sadaka kondoo na ng'ombe, wasioweza kuhesabiwa wala idadi yao kujulikana kwa kuwa wengi. Makuhani wakalileta sanduku la Agano la BWANA hadi mahali pake, katika chumba cha ndani cha ile nyumba, patakatifu pa patakatifu, naam, chini ya mbawa za makerubi. Kwa maana makerubi yalinyosha mbawa zao, juu ya mahali pa sanduku, makerubi yakalifunika lile sanduku na miti yake kwa juu. Na ile miti kwa kuwa mirefu, ncha za miti zilionekana katika mahali patakatifu, mbele ya chumba cha ndani; lakini hazikuonekana nje; nayo iko kuko huko hata leo. Hamkuwa na kitu ndani ya sanduku, ila zile mbao mbili za mawe ambazo Musa aliziweka ndani huko Horebu, BWANA alipofanya agano na wana wa Israeli, hapo walipotoka katika nchi ya Misri. Ikawa, makuhani walipotoka katika patakatifu, nyumba ya BWANA ikajaa wingu; hata makuhani hawakuweza kusimama ili kufanya huduma yao, kwa sababu ya wingu lile; kwa kuwa nyumba ya BWANA ilikuwa imejaa utukufu wa BWANA.

1 Wafalme 8:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kisha Mfalme Solomoni akawaita mbele zake huko Yerusalemu wazee wa Israeli, viongozi wote wa makabila na wakuu wa jamaa za Waisraeli, ili walilete Sanduku la Agano la BWANA kutoka Sayuni, Mji wa Daudi. Wanaume wote wa Israeli wakakusanyika kwa Mfalme Solomoni wakati wa sikukuu ya mwezi wa Ethanimu, ndio mwezi wa saba. Wazee wote wa Israeli walipofika, makuhani wakajitwika Sanduku la Agano, nao wakalipandisha Sanduku la BWANA, na Hema la Kukutania pamoja na vyombo vyote vitakatifu vilivyokuwa ndani yake. Makuhani na Walawi wakavibeba, naye Mfalme Solomoni na kusanyiko lote la Israeli waliokusanyika kumzunguka walikuwa mbele ya hilo Sanduku, nao wakatoa dhabihu nyingi za kondoo na ngʼombe ambao idadi yao haikuwezekana kuandikwa au kuhesabiwa. Makuhani wakalileta Sanduku la Agano la BWANA hadi mahali pake ndani ya sehemu takatifu ndani ya Hekalu, yaani Patakatifu pa Patakatifu, na kuliweka chini ya mabawa ya makerubi. Makerubi yalitandaza mabawa yao juu ya mahali pa Sanduku la Agano na kutia kivuli Sanduku pamoja na mipiko yake ya kubebea. Mipiko hiyo ilikuwa mirefu sana kiasi kwamba ncha zake zilionekana kutoka Mahali Patakatifu mbele ya Patakatifu pa Patakatifu, lakini sio nje ya Mahali Patakatifu. Hiyo mipiko ipo hata leo. Ndani ya Sanduku hapakuwepo kitu kingine chochote isipokuwa zile mbao mbili za mawe ambazo Mose alikuwa ameziweka ndani yake huko Horebu, mahali ambapo BWANA alifanya Agano na Waisraeli baada ya kutoka Misri. Makuhani walipoondoka katika Mahali Patakatifu, wingu likajaza Hekalu la BWANA. Nao makuhani hawakuweza kufanya huduma yao kwa sababu ya lile wingu, kwa kuwa utukufu wa BWANA ulijaza Hekalu lake.