1 Wafalme 7:40-51
1 Wafalme 7:40-51 SRUV
Tena Huramu akazifanya birika, na majembe, na mabakuli. Hivyo Huramu akazimaliza kazi zote alizomfanyia mfalme Sulemani katika nyumba ya BWANA; zile nguzo mbili, na mabakuli mawili ya mataji yalikuwa juu ya nguzo; na nyavu mbili za kuvifunika hivyo viumbe viwili vya mataji yaliyokuwa juu ya nguzo; na makomamanga mia nne ya zile nyavu mbili; safu mbili za makomamanga kwa kila wavu, kuyafunika nayo mabakuli mawili ya mataji yaliyokuwa juu ya nguzo; na vile vitako kumi, na birika kumi juu ya vitako; na ile bahari moja, na ng'ombe kumi na wawili chini ya ile bahari; na masufuria, na majembe, na mabeseni; hata vyombo hivyo vyote, Huramu alivyomfanyia mfalme Sulemani, katika nyumba ya BWANA, vyote vilikuwa vya shaba iliyosuguliwa. Katika uwanda wa Yordani ndipo mfalme alipovisubu, katika udongo mzito kati ya Sukothi na Sarethani. Sulemani akaviacha vyombo vyote visipimwe kwa kuwa vilikuwa vingi mno; wala uzito wa shaba haukujulikana. Sulemani akavitengeneza vyombo vyote vilivyokuwamo nyumbani mwa BWANA; madhabahu ya dhahabu, na ile meza iliyokuwa na mikate ya wonyesho juu yake ilikuwa ya dhahabu; na vinara vya taa, vitano upande wa kulia, na vitano upande wa kushoto, mbele ya chumba cha ndani, vya dhahabu safi; na maua, na taa, na koleo ya dhahabu; na vikombe, na makasi, na mabakuli, na miiko, na vyetezo, vya dhahabu safi; na bawaba za dhahabu, za milango ya nyumba ya ndani, yaani, patakatifu pa patakatifu, na za milango ya nyumba, ndiyo hekalu. Hivyo kazi yote aliyoifanya mfalme Sulemani katika nyumba ya BWANA ikamalizika. Sulemani akaviingiza vile vitu alivyovitakasa Daudi baba yake, yaani, fedha, na dhahabu, na vyombo; akavitia ndani ya hazina za nyumba ya BWANA.