1 Wakorintho 15:35-49
1 Wakorintho 15:35-49 SRUV
Lakini labda mtu atasema, Wafu wafufuliwaje? Nao huja kwa mwili gani? Ewe mpumbavu! Uipandayo haihuiki, isipokufa; nayo uipandayo, huupandi mwili ule utakaokuwa, ila chembe tupu, ikiwa ni ya ngano au nyingineyo; lakini Mungu huipa mwili kama apendavyo, na kila mbegu mwili wake. Nyama zote hazifanani; nyingine ni ya wanadamu, nyingine ya hayawani, nyingine ya ndege, nyingine ya samaki. Tena kuna miili ya mbinguni, na miili ya duniani; lakini fahari yake ile ya mbinguni ni mbali, na fahari yake ile ya duniani ni mbali. Kuna fahari moja ya jua, na fahari nyingine ya mwezi, na fahari nyingine ya nyota; maana iko tofauti ya fahari hata kati ya nyota na nyota. Hivyo ndivyo ilivyo kwa kiyama ya wafu. Hupandwa katika uharibifu; hufufuliwa katika kutoharibika; hupandwa katika aibu; hufufuliwa katika fahari; hupandwa katika udhaifu; hufufuliwa katika nguvu; hupandwa mwili wa asili; hufufuliwa mwili wa roho. Ikiwa uko mwili wa asili, na wa roho pia uko. Ndivyo ilivyoandikwa, Mtu wa kwanza, Adamu, akawa kiumbe aliye hai; Adamu wa mwisho ni roho yenye kuhuisha. Lakini hautangulii ule wa roho, bali ule wa asili; baadaye huja ule wa roho. Mtu wa kwanza atoka katika nchi, ni wa udongo. Mtu wa pili atoka mbinguni. Kama alivyo yeye wa udongo, ndivyo walivyo walio wa udongo; na kama alivyo yeye wa mbinguni, ndivyo walivyo walio wa mbinguni. Na kama tulivyoichukua sura yake yule wa udongo, kadhalika tutaichukua sura yake yeye aliye wa mbinguni.