Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Mambo ya Nyakati 15:1-16

1 Mambo ya Nyakati 15:1-16 SRUV

Basi Daudi akajijengea nyumba katika mji wa Daudi; akatayarisha mahali kwa ajili ya sanduku la Mungu, akalipigia hema. Ndipo Daudi akasema, Haimpasi mtu awaye yote kulichukua sanduku la Mungu, isipokuwa Walawi peke yao; kwa kuwa hao ndio aliowachagua BWANA, ili walichukue sanduku la Mungu, na kumtumikia daima. Basi Daudi akawakusanya Israeli wote huko Yerusalemu, ili kulipandisha sanduku la BWANA, mpaka mahali pake alipoliwekea tayari. Daudi akawakutanisha wana wa Haruni, na Walawi; wa wana wa Kohathi; Urieli mkuu wao, na nduguze mia moja na ishirini; wa wana wa Merari; Asaya mkuu wao, na nduguze mia mbili na ishirini; wa wana wa Gershoni; Yoeli mkuu wao, na nduguze mia moja na thelathini; wa wana wa Elsafani; Shemaya mkuu wao, na nduguze mia mbili; wa wana wa Hebroni; Elieli mkuu wao, na nduguze themanini; wa wana wa Uzieli; Aminadabu mkuu wao, na nduguze mia moja kumi na wawili. Tena, Daudi akawaita Sadoki na Abiathari makuhani, na hao Walawi, Urieli, Asaya, Yoeli, Shemaya, Elieli, na Aminadabu, akawaambia, Ninyi ni vichwa vya koo za baba za Walawi; jitakaseni, ninyi na ndugu zenu, ili mlipandishe sanduku la BWANA, Mungu wa Israeli, mpaka mahali pale nilipolitayarishia. Kwa kuwa ninyi hamkulichukua safari ya kwanza, BWANA, Mungu wetu, alitufurikia, kwa maana hatukumtafuta kulingana na sheria. Basi makuhani na Walawi wakajitakasa, ili wapate kulipandisha sanduku la BWANA, Mungu wa Israeli. Na wana wa Walawi wakalichukua sanduku la Mungu mabegani mwao kwa miti yake, kama vile Musa alivyoamuru, kulingana na neno la BWANA. Kisha Daudi akamwambia mkuu wa Walawi, kwamba awaagize ndugu zao waimbaji, pamoja na vyombo vyao vya kupigia ngoma, vinanda, na vinubi, na matoazi, wavipige na kupaza sauti kwa furaha.