Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wamakabayo 15

15
Ufedhuli wa Nikano
1Nikano aliposikia ya kuwa Yuda na watu wake wako katika nchi ya Samaria, alifanya shauri kuwashambulia bila hatari siku ya kupumzika. 2Wayahudi walioshurutishwa kufuatana naye walisema, Usiharibu hivi kwa ukatili na ushenzi; iadhimishe siku ambayo Yeye avitazamaye vyote ameiadhimisha na kuitakasa. 3Naye yule mwenye kulaaniwa mara tatu akauliza kama yupo mfalme mbinguni aliyeamuru Sabato ishikwe. 4Wakamjibu, Kuna BWANA aliye hai, Mfalme mwenyewe mbinguni ndiye aliyetuagiza tuishike siku ya saba. 5Akasema, Mimi nami ni mfalme hapa duniani, na amri yangu ndiyo mshike silaha na kufanya kazi ya mfalme. Lakini hakufaulu katika kulitimiza shauri lake baya.
Yuda awaandaa Wayahudi
6Basi Nikano, hali moyo wake umejaa kiburi, alinuia kusimamisha nguzo ya ukumbusho wa ushindi wake juu ya Yuda na watu wake. 7Hata hivi, Makabayo hakuacha kutumaini kwa imani kabisa ya kuwa atapata msaada kwa BWANA. 8Akawaonya watu wake wasiyaogope mashambulio ya mataifa, bali waukumbuke msaada walioupata mara nyingi kutoka mbinguni na kuutazamia sasa ushindi watakaoletewa na Mwenyezi. 9Akawafariji kwa maneno ya Sheria na Manabii, na kuwakumbusha ushindi wao katika mapigano mengi, na hivyo aliwatia moyo. 10Akiisha kuwakuza moyo aliwapa maagizo yake akiwakumbusha uhaini wa watu wa mataifa, na jinsi wavunjavyo viapo vyao. 11Alimvika kila mtu nguvu – siyo matumaini yaliyowekwa kwa ngao na mikuki, bali ushujaa uletwao kwa maneno mema. 12Zaidi ya hayo, aliwachangamsha kwa kuwasimulia njozi iliyostahili kusadikiwa, maono ya namna hii: Alimwona Oniasi, yule aliyekuwa kuhani mkuu zamani, mtu mwema, muungwana, msharifu lakini mpole, mwenye maneno mazuri, aliyelelewa vizuri tangu utoto wake katika wema wote. 13Akatokea mtu mwingine, amesimama vivi hivi, amebainika kwa mvi zake na kwa utukufu wake, amevikwa adhama ya ajabu. 14Oniasi, akasema, Huyu ni mpenda ndugu, mwenye kuwaombea kwa bidii sana watu wa mji mtakatifu; ndiye Yeremia, nabii wa Mungu. 15Yeremia akaunyosha mkono wake wa kuume, akampa Yuda upanga wa dhahabu na huku akimwambia, 16Pokea upanga huu mtakatifu uliopewa na Mungu; kwao utawapiga adui.
Maitikio ya askari
17Wakatiwa moyo kwa maneno ya Yuda, maana yalikuwa maneno bora, ya kuchochea tamaa ya wema na kuamsha ushujaa wa kiume katika mioyo ya vijana; wakakata shauri wasikae kambini, bali waende mbele bila hofu na kupigana na adui mkono kwa mkono mpaka ijulikane ni nani watakaoshinda; kwa sababu mji na mahali patakatifu na hekalu vimo katika hatari. 18Hofu yao kwa ajili ya wake zao na wana wao, na kwa ndugu zao pia na jamaa zao, ilikuwa si jambo zito kwao kama hofu yao kuu, iliyopita yote, kwa ajili ya hekalu takatifu. 19Nao waliokuwa mjini waliona kiherehere juu ya mapigano yanayofanyika nje, wakihangaika sana.
20Basi, wote walikuwa wakingojea matokeo ya mashindano. Adui walikuwa wamekusanyana na kujipanga tayari kwa vita; tembo wamewekwa mahali pa kufaa, na wapanda farasi kandokando. 21Makabayo akatazama majeshi makubwa mbele yake, na silaha zao za kila namna, na tembo wakali, akanyosha mikono yake kuelekea mbinguni akamsihi BWANA atendaye miujiza, maana alijua ya kuwa ushindi hauji kwa silaha, ila ni Mungu anayewapa wao walioustahili. 22#2 Fal 19:35 Maombi yake yalikuwa hivi; Wewe, BWANA, Mfalme mkuu, zamani za Hezekia, mfalme wa Uyahudi, ulimpeleka malaika wako akaua watu mia themanini na elfu tano wa jeshi la Senakeribu. 23Basi, sasa pia, Ee Mfalme wa mbinguni, upeleke malaika mwema mbele yetu kutisha na kuogofya. 24Na kwa uweza wa mkono wako uwafadhaishe hawa wanaokuja kwa makufuru juu ya hekalu lako takatifu.
Kushindwa kwa Nikano na kifo chake
25 # 1 Mak 7:43-50 Alipoyamaliza maneno hayo, Nikano na majeshi yake walianza mashambulio yao kwa tarumbeta na nyimbo za shangwe; 26hali Yuda na watu wake waliwapokea adui wakimwitia Mungu na kuomba. 27Kwa mikono yao walipigana, na kwa mioyo yao walimwomba Mungu; na hivi waliua watu wasiopungua elfu thelathini na tano, wakifurahishwa sana kwa msaada dhahiri wa Mungu. 28Baada ya mapigano, walipokuwa wakirudi kwa furaha, walimwona Nikano, amevaa silaha zake zote, amelala chini amekufa. 29Wakapaza sauti zao kwa shangwe, wakimsifu Mfalme mkuu kwa lugha za wazee wao. 30Yeye, aliyekuwa tayari sikuzote, mwili na roho, kuwashindania Wayahudi wenzake, aliyehifadhi katika maisha yake yote ile nia njema kwao ya ujana wake, aliwaagiza wakate kichwa cha Nikano na mkono wake penye bega na kuvipeleka Yerusalemu. 31Walipofika alikusanya watu na kuwaweka makuhani mbele ya madhabahu, kisha aliagiza wale wa ngomeni waitwe. 32Akawaonesha kichwa cha yule mlaaniwa Nikano, na mkono wake yule mkufuru aliokuwa ameunyosha kwa kiburi juu ya nyumba takatifu ya Mwenyezi. 33Akaukata ulimi wa yule mwovu Nikano, akasema atautupia kwa ndege vipande vipande, na kutungika mapato ya ujinga wake kupaelekea patakatifu. 34Wote wakapaza sauti zao mbinguni wakimhimidi BWANA aliyejifunua, wakisema; Ahimidiwe Yeye aliyepalinda mahali pake pasitiwe unajisi. 35Akakitungika kichwa cha Nikano ngomeni kiwe ushuhuda dhahiri, wazi kwa wote, wa msaada wa BWANA. 36#1 Mak 7:49 Nao wote pamoja wakakata shauri na kutangaza amri ya kuwa siku hii isisahauliwe kamwe, bali siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili – uitwao Adari kwa lugha ya Kishamu – yaani ile siku kabla ya Siku ya Mordekai, iwe sikukuu ya kuadhimishwa.
Maneno ya Mwisho ya Mtungaji
37Hizo ndizo habari za Nikano. Tangu wakati ule mji umekuwa mikononi mwa Wayahudi; kwa hiyo mimi nami nitayakomesha masimulizi yangu hapo.
38Kama yametungwa kwa ufasaha na kupangwa kwa ustadi, ndivyo nilivyotaka. Lakini kama ni hafifu, au si mazuri sana, ndivyo nilivyoweza. 39Kama vile haifai kunywa divai peke yake, au maji peke yake, ila divai iliyochanganywa na maji ina afya na kupendeza; ndivyo masimulizi mazuri yakitungwa kwa ufasaha, huyafurahisha masikio yao wanaoyasoma.
Na yakome hapa.

Iliyochaguliwa sasa

2 Wamakabayo 15: SRUVDC

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia