Rum 15:22-33
Rum 15:22-33 SUV
Ndiyo sababu nalizuiwa mara nyingi nisije kwenu. Lakini sasa, kwa kuwa sina wasaa tena pande hizi, tena tangu miaka mingi nina shauku kuja kwenu; wakati wo wote nitakaosafiri kwenda Spania [nitakuja kwenu.] Kwa maana nataraji kuwaona ninyi katika kusafiri kwangu, na kusafirishwa nanyi, moyo wangu ushibe kwenu kidogo. Ila sasa ninakwenda Yerusalemu, nikiwahudumu watakatifu; maana imewapendeza watu wa Makedonia na Akaya kufanya changizo kwa ajili ya watakatifu huko Yerusalemu walio maskini. Naam, imewapendeza, tena wamekuwa wadeni wao. Kwa maana ikiwa Mataifa wameyashiriki mambo yao ya roho, imewabidi kuwahudumu kwa mambo yao ya mwili. Basi nikiisha kuimaliza kazi hiyo, na kuwatilia muhuri tunda hilo, nitapitia kwenu, kwenda Spania. Nami najua ya kuwa nikija kwenu nitakuja kwa utimilifu wa baraka ya Kristo. Ndugu zangu, nawasihi kwa Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa upendo wa Roho, jitahidini pamoja nami katika maombi yenu kwa ajili yangu mbele za Mungu; kwamba niokolewe na wale wasioamini katika Uyahudi, na tena huduma yangu niliyo nayo huko Yerusalemu ikubalike kwa watakatifu; nipate kufika kwenu kwa furaha, kama apendavyo Mungu, nikapate kupumzika pamoja nanyi. Mungu wa amani na awe pamoja nanyi nyote. Amina.