Zab 37:1-15
Zab 37:1-15 SUV
Usikasirike kwa sababu ya watenda mabaya, Usiwahusudu wafanyao ubatili. Maana kama majani watakatika mara, Kama miche mibichi watanyauka. Umtumaini BWANA ukatende mema, Ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu. Nawe utajifurahisha kwa BWANA, Naye atakupa haja za moyo wako. Umkabidhi BWANA njia yako, Pia umtumaini, naye atafanya. Ataitokeza haki yako kama nuru, Na hukumu yako kama adhuhuri. Ukae kimya mbele za BWANA, Nawe umngojee kwa saburi; Usimkasirikie yeye afanikiwaye katika njia yake, Wala mtu afanyaye hila. Ukomeshe hasira, uache ghadhabu, Usikasirike, mwisho wake ni kutenda mabaya. Maana watenda mabaya wataharibiwa, Bali wamngojao BWANA ndio watakaoirithi nchi. Maana bado kitambo kidogo asiye haki hatakuwapo, Utapaangalia mahali pake wala hatakuwapo. Bali wenye upole watairithi nchi, Watajifurahisha kwa wingi wa amani. Asiye haki hunuia mabaya juu ya mwenye haki, Na kumsagia meno yake. BWANA atamcheka, Maana ameona kwamba siku yake inakuja. Wasio haki wamefuta upanga na kupinda uta, Wamwangushe chini maskini na mhitaji, Na kuwaua wenye mwenendo wa unyofu. Upanga wao utaingia mioyoni mwao wenyewe, Na nyuta zao zitavunjika.