Mit 25:1-13
Mit 25:1-13 SUV
Hizi nazo ni mithali za Sulemani, ambazo watu wa Hezekia, mfalme wa Yuda, walizinakili. Ni utukufu wa Mungu kuficha jambo; Bali ni utukufu wa mfalme kuchunguza jambo. Mbingu huenda juu sana, na nchi huenda chini; Lakini mioyo ya wafalme haichunguziki. Ondoa takataka katika fedha, Na chombo kitatokea kwa mtakasaji; Mwondoe asiye haki mbele ya mfalme, Na kiti chake cha enzi kitathibitika katika haki. Usijitukuze mbele ya uso wa mfalme; Wala usisimame mahali pa watu wakuu; Kwa maana ni heri kuambiwa, Njoo huku mbele; Kuliko kuwekwa nyuma machoni pa mkuu. Yale uliyoyaona kwa macho, Usitoke nje kwa haraka ili kuyashindania; Usije ukakosa kujua la kutenda hatimaye, Mwenzako atakapokuwa amekuaibisha. Ujitetee na mwenzako peke yake; Bali usiifunue siri ya mtu mwingine; Yeye asikiaye asije akakutukana; Na aibu yako isiondoke. Neno linenwalo wakati wa kufaa, Ni kama machungwa katika vyano vya fedha. Kipuli cha dhahabu, na pambo la dhahabu safi; Ndivyo alivyo mwonyaji mwenye hekima kwa sikio lisikialo. Kama baridi ya theluji wakati wa mavuno; Ndivyo alivyo mjumbe mwaminifu kwao wamtumao; Kwa maana huwaburudisha bwana zake nafsi zao.