Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mit 10:1-32

Mit 10:1-32 SUV

Mwana mwenye hekima humfurahisha babaye; Bali mwana mpumbavu ni mzigo wa mamaye. Hazina za uovu hazifaidii kitu; Bali haki huokoa na mauti. BWANA hataiacha nafsi ya mwenye haki ife na njaa; Bali tamaa ya mtu mwovu huisukumia mbali. Atendaye mambo kwa mkono mlegevu huwa maskini; Bali mkono wake aliye na bidii hutajirisha. Akusanyaye wakati wa hari ni mwana mwenye hekima; Bali asinziaye wakati wa mavuno ni mwana mwenye kuaibisha. Baraka humkalia mwenye haki kichwani; Bali jeuri hufunika kinywa chake mtu mwovu. Kuwakumbuka wenye haki huwa na baraka; Bali jina la mtu mwovu litaoza. Aliye na akili moyoni mwake atapokea agizo; Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka. Aendaye kwa unyofu huenda salama; Bali apotoshaye njia zake atajulikana. Akonyezaye kwa jicho huleta masikitiko; Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka. Kinywa chake mwenye haki ni chemchemi ya uzima; Bali jeuri hufunika kinywa chake mtu mwovu, Kuchukiana huondokesha fitina; Bali kupendana husitiri makosa yote. Hekima hupatikana midomoni mwa mwenye ufahamu; Bali fimbo hufaa kwa mgongo wake asiye na ufahamu. Watu wenye akili huweka akiba ya maarifa; Bali kinywa cha mpumbavu ni uangamivu ulio karibu. Mali ya mtu tajiri ni mji wake wa nguvu; Uangamivu wa maskini ni umaskini wao. Kazi yake mwenye haki huuelekea uzima; Mazao ya wabaya huuelekea dhambi. Akubaliye kurudiwa huwa katika njia ya uzima; Bali yeye aachaye maonyo hukosa. Yeye afichaye chuki ana midomo ya uongo, Na yeye asingiziaye ni mpumbavu. Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu; Bali yeye azuiaye midomo yake hufanya akili. Ulimi wa mwenye haki ni kama fedha teule; Moyo wa mtu mbaya haufai kitu. Midomo ya mwenye haki hulisha watu wengi; Bali wapumbavu hufa kwa kuwa hawana ufahamu. Baraka ya BWANA hutajirisha, Wala hachanganyi huzuni nayo. Kwa mpumbavu kutenda maovu ni kama mchezo; Bali mtu mwenye ufahamu ana hekima. Aogopacho mtu asiye haki ndicho kitakachomjilia; Na wenye haki watapewa matakwa yao. Kisulisuli kikiisha pita asiye haki hayuko tena; Bali mwenye haki ni msingi wa milele. Kama siki menoni, na kama moshi machoni, Ndivyo alivyo mtu mvivu kwao wamtumao. Kumcha BWANA kwaongeza siku za mtu; Bali miaka yao wasio haki itapunguzwa. Matumaini yao wenye haki yatakuwa furaha; Bali kutaraji kwao wasio haki kutapotea. Njia ya BWANA ni kimbilio lake mtu mkamilifu; Bali ni uharibifu kwao watendao maovu. Mwenye haki hataondolewa milele; Bali wasio haki hawatakaa katika nchi. Kinywa cha mwenye haki hutoa hekima; Bali ulimi wa ukaidi utakatiliwa mbali. Midomo ya mwenye haki huyajua yatakayokubaliwa; Bali kinywa chao wasio haki hunena ukaidi.

Soma Mit 10