Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hes 20:1-13

Hes 20:1-13 SUV

Kisha wana wa Israeli, mkutano wote, wakaingia bara ya Sini, katika mwezi wa kwanza, watu wakakaa Kadeshi; Miriamu akafa huko, akazikwa huko. Na hapo hapakuwa na maji kwa ule mkutano; wakajikusanya juu ya Musa na juu ya Haruni. Watu wakashindana na Musa, wakanena, wakisema, Ingalikuwa heri kama tungalikufa wakati ule ndugu zetu walipokufa mbele za BWANA! Mbona mmewaleta kusanyiko la BWANA hata jangwa hili ili tufe huku, sisi na wanyama wetu? Na mbona mmetupandisha kutoka Misri ili kutuleta hata mahali hapa pabaya? Si mahali pa mbegu, wala tini, wala mizabibu, wala makomamanga; wala hapana maji ya kunywa. Musa na Haruni wakatoka pale palipokuwa mkutano, wakaenda hata mlangoni pa hema ya kukutania, wakaanguka kifudifudi; utukufu wa BWANA ukawatokea. BWANA akasema na Musa, akinena, Twaa ile fimbo, ukawakusanye mkutano, wewe na Haruni ndugu yako, ukauambie mwamba mbele ya macho yao utoe maji yake, nawe utawatokezea maji katika mwamba, na hivyo utawanywesha maji mkutano na wanyama wao. Musa akaitwaa hiyo fimbo kutoka mbele za BWANA kama alivyomwamuru. Musa na Haruni wakawakusanya kusanyiko mbele ya mwamba, akawaambia, Sikieni sasa, enyi waasi; je! Tuwatokezee maji katika mwamba huu? Musa akainua mkono wake akaupiga ule mwamba kwa fimbo yake mara mbili; maji yakatoka mengi, mkutano wakanywa na wanyama wao pia. BWANA akamwambia Musa na Haruni, Kwa kuwa hamkuniamini mimi, ili kunistahi mbele ya macho ya wana wa Israeli, basi kwa sababu hiyo, hamtawaingiza kusanyiko hili katika ile nchi niliyowapa. Maji haya ni maji ya Meriba; kwa sababu wana wa Israeli waliteta na BWANA, naye alijionyesha kuwa mtakatifu kati yao.