Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Nah 2

2
Maangamizi ya Mji Mwovu
1Yeye asetaye vipande vipande amepanda juu mbele ya uso wako; zishike silaha, ilinde njia, vitie nguvu viuno vyako, uongeze uwezo wako sana. 2Kwa maana BWANA anairudisha fahari ya Yakobo, kama fahari ya Israeli; maana watekao nyara wamewateka, na kuyaharibu matawi ya mizabibu yao. 3Ngao ya mashujaa wake imefanywa kuwa nyekundu, watu walio hodari wa vita wamevaa nguo nyekundu sana; magari ya vita yametameta kwa chuma cha pua siku ya kujitengeza kwake, na mikuki inatikiswa kwa namna ya kutisha.
4Magari ya vita yanafanya mshindo njiani,
Yanasongana-songana katika njia kuu;
Kuonekana kwake ni kama mienge,
Yanakwenda upesi kama umeme.
5Awakumbuka watu wake wenye heshima;
Wanajikwaa katika mwendo wao;
Wanafanya haraka waende ukutani;
Nacho kitu cha kuwafunika kimewekwa tayari.
6Malango ya mito yamefunguka, na jumba la mfalme limeyeyushwa. 7Husabu naye amefunuliwa, anachukuliwa, na wajakazi wake wanalia kama kwa sauti ya hua, wakipiga-piga vifua vyao. 8Lakini Ninawi tokea zamani amekuwa kama ziwa la maji; ila hata sasa wanakimbia; Simameni! Simameni! Lakini hapana hata mmoja atazamaye nyuma.
9Chukueni nyara za fedha;
Chukueni nyara za dhahabu;
Kwa maana ni akiba isiyoisha,
Fahari ya vyombo vipendezavyo.
10Amekuwa utupu, na ukiwa, na uharibifu; hata moyo unayeyuka, na magoti yanagongana-gongana; viunoni mwote mna utungu, na nyuso za wote zimekuwa nyeupe kwa hofu.
11Kao la simba li wapi? Na mahali walishapo wana-simba pa wapi, mahali walipotembea simba mume na simba mke na mwana-simba, wala hapana aliyewatia hofu? 12Simba alirarua vipande vipande chakula cha kuwatosha watoto wake, aliwasongea wake zake nyama, aliyajaza mapango yake mateka, na makao yake aliyajaza mawindo.
13Tazama, mimi ni juu yako, asema BWANA wa majeshi, nami nitayateketeza magari yako ya vita katika moshi, na upanga utawala wana-simba wako; nami nitayakatilia mbali mawindo yako katika nchi, na sauti za wajumbe wako hazitasikiwa tena kamwe.

Iliyochaguliwa sasa

Nah 2: SUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia