Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mk 14:53-65

Mk 14:53-65 SUV

Nao wakamchukua Yesu kwa Kuhani Mkuu; wakamkusanyikia wote, wakuu wa makuhani na wazee na waandishi. Naye Petro akamfuata kwa mbali, hata ndani katika behewa ya Kuhani Mkuu; akawa ameketi pamoja na watumishi, anakota moto mwangani. Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda juu ya Yesu wapate kumwua; wasione. Kwa maana wengi walimshuhudia uongo, walakini ushuhuda wao haukupatana. Hata wengine wakasimama, wakamshuhudia uongo, wakisema, Sisi tulimsikia akisema, Mimi nitalivunja hekalu hili lililofanyika kwa mikono, na katika siku tatu nitajenga jingine lisilofanyika kwa mikono. Wala hata hivi ushuhuda wao haukupatana. Kisha Kuhani Mkuu akasimama katikati, akamwuliza Yesu, akisema, Hujibu neno? Hawa wanakushuhudia nini? Lakini akanyamaza, wala hakujibu neno. Kuhani Mkuu akamwuliza tena, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wake Mtukufu? Yesu akasema, Mimi ndiye, nanyi mtamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija na mawingu ya mbinguni. Kuhani Mkuu akararua nguo zake, akisema, Tuna haja gani tena ya mashahidi? Mmesikia kufuru yake; mwaonaje ninyi? Wote wakamhukumu kuwa imempasa kuuawa. Wengine wakaanza kumtemea mate, wakamfunika uso, na kumpiga makonde, na kumwambia, tabiri. Hata watumishi nao wakampiga makofi.