Mt 27:11-31
Mt 27:11-31 SUV
Naye Yesu akasimama mbele ya liwali; liwali akamwuliza, akasema, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Yesu akamwambia, Wewe wasema. Lakini aliposhitakiwa na wakuu wa makuhani na wazee, hakujibu hata neno. Ndipo Pilato akamwambia, Husikii ni mambo mangapi wanayokushuhudia? Asimjibu hata neno moja, hata liwali akastaajabu sana. Basi wakati wa siku kuu, liwali desturi yake huwafungulia mkutano mfungwa mmoja waliyemtaka. Basi palikuwa na mfungwa mashuhuri siku zile, aitwaye Baraba. Basi walipokutanika, Pilato akawaambia, Mnataka niwafungulie yupi? Yule Baraba, au Yesu aitwaye Kristo? Kwa maana alijua ya kuwa wamemtoa kwa husuda. Na alipokuwa ameketi juu ya kiti cha hukumu, mkewe alimpelekea mjumbe, kumwambia, Usiwe na neno na yule mwenye haki; kwa sababu nimeteswa mengi leo katika ndoto kwa ajili yake. Nao wakuu wa makuhani na wazee wakawashawishi makutano ili wamtake Baraba, na kumwangamiza Yesu. Basi liwali akajibu, akawaambia, Mnataka niwafungulie yupi katika hawa wawili? Wakasema, Baraba. Pilato akawaambia, Basi, nimtendeje Yesu aitwaye Kristo? Wakasema wote, Asulibiwe. Akasema, Kwani? Ni ubaya gani alioutenda? Wakazidi sana kupiga kelele, wakisema, Na asulibiwe. Basi Pilato alipoona ya kuwa hafai lo lote, bali ghasia inazidi tu, akatwaa maji, akanawa mikono yake mbele ya mkutano, akasema, Mimi sina hatia katika damu ya mtu huyu mwenye haki; yaangalieni haya ninyi wenyewe. Watu wote wakajibu wakasema, Damu yake na iwe juu yetu, na juu ya watoto wetu. Ndipo akawafungulia Baraba; na baada ya kumpiga Yesu mijeledi, akamtoa ili asulibiwe. Ndipo askari wa liwali wakamchukua Yesu ndani ya Praitorio, wakamkusanyikia kikosi kizima. Wakamvua nguo, wakamvika vazi jekundu. Wakasokota taji ya miiba, wakaiweka juu ya kichwa chake, na mwanzi katika mkono wake wa kuume; wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki, wakisema, Salamu, Mfalme wa Wayahudi! Kisha wakamtemea mate, wakautwaa ule mwanzi, wakampiga-piga kichwani. Walipokwisha kumdhihaki, wakalivua lile vazi, wakamvika mavazi yake, wakamchukua kumsulibisha.