Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mt 17:14-27

Mt 17:14-27 SUV

Nao walipoufikia mkutano, mtu mmoja akamjia, akampigia magoti, akisema, Bwana, umrehemu mwanangu, kwa kuwa ana kifafa, na kuteswa vibaya; maana mara nyingi huanguka motoni, na mara nyingi majini. Nikamleta kwa wanafunzi wako, wasiweze kumponya. Yesu akajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, kilichopotoka, nitakaa pamoja nanyi hata lini? Nitachukuliana nanyi hata lini? Mleteni huku kwangu. Yesu akamkemea pepo, naye akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile. Kisha wale wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha wakasema Mbona sisi hatukuweza kumtoa? Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu. [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.] Nao walipokuwa wakikaa Galilaya, Yesu akawaambia, Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua, na siku ya tatu atafufuka. Wakasikitika sana. Hata walipofika Kapernaumu, wale watozao nusu-shekeli walimwendea Petro, wakasema, Je! Mwalimu wenu hatoi nusu-shekeli? Akasema, Hutoa. Naye alipoingia nyumbani, Yesu alitangulia kumwuliza, akisema, Waonaje, Simoni? Wafalme wa dunia hutwaa kodi ama ushuru kwa watu gani? Kwa wana wao au kwa wageni? Naye aliposema, Kwa wageni, Yesu alimwambia, Basi, kama ni hivyo, wana ni mahuru. Lakini tusije tukawakwaza, enenda baharini ukatupe ndoana, ukatwae samaki yule azukaye kwanza; na ukifumbua mdomo wake utaona shekeli; ichukue hiyo ukawape kwa ajili yangu na kwa ajili yako.

Soma Mt 17

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mt 17:14-27