Lk 9:1-17
Lk 9:1-17 SUV
Akawaita wale Thenashara, akawapa uwezo na mamlaka juu ya pepo wote na kuponya maradhi. Akawatuma wautangaze ufalme wa Mungu, na kupoza wagonjwa. Akawaambia, Msichukue kitu kwa safari yenu, fimbo, wala mkoba, wala mkate, wala fedha, wala mmoja wenu asiwe na kanzu mbili. Na nyumba yo yote mtakayoingia kaeni humo, mpaka mtoke mjini. Na wale wasiowakaribisha, mtokapo katika mji huo, yakung’uteni hata mavumbi ya miguuni mwenu, kuwa ushuhuda juu yao. Wakaenda, wakazunguka katika vijiji, wakihubiri injili, na kupoza watu kila mahali. Na Herode mfalme akasikia habari za yote yaliyotendeka, akafadhaika kwa sababu watu wengine walisema ya kwamba Yohana amefufuka katika wafu, na wengine ya kwamba Eliya ametokea, na wengine ya kwamba mmojawapo wa manabii wa kale amefufuka. Lakini Herode akasema, Yohana nilimkata kichwa; basi ni nani huyu ambaye ninasikia mambo haya juu yake? Akataka kumwona. Basi wale mitume waliporudi walimweleza mambo yote waliyoyatenda; akawachukua, akaenda nao faraghani mpaka mji mmoja uitwao Bethsaida. Na makutano walipojua walimfuata; akawakaribisha, akawa akisema nao habari za ufalme wa Mungu, akawaponya wale wenye haja ya kuponywa. Na jua likaanza kushuka; wakamwendea wale Thenashara, wakamwambia, Uage mkutano, ili waende katika vijiji na mashamba ya kandokando wapate mahali pa kulala na vyakula, maana hapa tulipo ni nyika tupu. Akawaambia, Wapeni ninyi chakula. Wakasema, Hatuna kitu zaidi ya mikate mitano na samaki wawili, tusipokwenda tukawanunulie watu hawa wote vyakula. Kwa kuwa wanaume waliokuwako walipata kama elfu tano. Akawaambia wanafunzi wake, Waketisheni watu kwa safu, kila safu watu hamsini. Wakafanya hivyo, wakawaketisha wote. Akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni akavibariki, akavimega, akawapa wanafunzi wake ili wawaandikie mkutano. Wakala, wakashiba wote; na katika vile vipande vilivyowabakia walikusanya vikapu kumi na viwili.