Lk 4:31-44
Lk 4:31-44 SUV
Akashuka mpaka Kapernaumu, mji wa Galilaya, akawa akiwafundisha siku ya sabato; wakashangaa mno kwa mafundisho yake, kwa kuwa neno lake lilikuwa na uwezo. Na ndani ya sinagogi mlikuwa na mtu mwenye roho ya pepo mchafu, akalia kwa sauti kuu, akisema, Acha! Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Umekuja kutuangamiza? Nakujua u nani, Mtakatifu wa Mungu. Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, mtoke. Ndipo yule pepo akamwangusha katikati, akamtoka asimdhuru neno. Mshangao ukawashika wote, wakasemezana wakisema, Ni neno gani hili, maana awaamuru pepo wachafu kwa uwezo na nguvu, nao hutoka. Habari zake zikaenea kila mahali katika nchi ile. Akatoka katika sinagogi, akaingia katika nyumba ya Simoni. Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa ameshikwa na homa kali, wakamwomba kwa ajili yake. Akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, ikamwacha; mara hiyo akaondoka, akawatumikia. Na jua lilipokuwa likichwa, wote waliokuwa na wagonjwa wenye maradhi mbali mbali waliwaleta kwake, akaweka mikono yake juu ya kila mmoja akawaponya. Pepo nao waliwatoka watu wengi, wakipiga kelele na kusema, Wewe u Mwana wa Mungu. Akawakemea, asiwaache kunena, kwa sababu walimjua kuwa ndiye Kristo. Hata kulipokucha alitoka akaenda mahali pasipokuwa na watu; makutano wakawa wakimtafuta-tafuta, wakafika kwake, wakataka kumzuia asiondoke kwao. Akawaambia, Imenipasa kuihubiri habari njema ya ufalme wa Mungu katika miji mingine pia; maana kwa sababu hiyo nalitumwa. Basi, alikuwa akihubiri katika masinagogi ya Galilaya.