Lk 11:29-54
Lk 11:29-54 SUV
Na makutano walipokuwa wakimkusanyikia, alianza kusema, Kizazi hiki ni kizazi kibaya; kinatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya Yona. Maana, kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa Waninawi, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu kwa kizazi hiki. Malkia wa Kusini ataondoka siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa na hatia; kwa sababu yeye alikuja kutoka ncha za dunia aisikie hekima ya Sulemani; na hapa pana mkubwa kuliko Sulemani. Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na kizazi hiki, nao watakihukumu kuwa na hatia; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona, na hapa pana mkubwa kuliko Yona. Hakuna mtu awashaye taa na kuiweka mahali palipositirika, au chini ya pishi; bali huiweka juu ya kiango, ili waingiao wapate kuuona mwanga. Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote unao mwanga; lakini likiwa bovu, mwili wako nao una giza. Angalia basi, mwanga ulio ndani yako usije ukawa giza. Basi kama mwanga umeenea katika mwili wako wote, wala hauna sehemu iliyo na giza, mwili wako wote utakuwa na mwanga mtupu; kama vile taa ikumulikiapo kwa mwanga wake. Alipokuwa akinena, Farisayo mmoja alimwita aje kwake ale chakula; akaingia, akaketi chakulani. Farisayo huyo alipomwona, alistaajabu kwa sababu hakunawa kabla ya chakula. Bwana akamwambia, Ninyi Mafarisayo mwasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani yenu mmejaa unyang’anyi na uovu. Enyi wapumbavu; aliyevifanya vya nje, siye yeye aliyevifanya vya ndani pia? Lakini, toeni sadaka vile vya ndani, na tazama, vyote huwa safi kwenu. Lakini, ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwatoa zaka za mnanaa na mchicha na kila mboga, na huku mwaacha mambo ya adili, na upendo wa Mungu; iliwapasa kuyafanya hayo ya kwanza, bila kuyaacha hayo ya pili. Ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwapenda kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni. Ole wenu, kwa kuwa mmefanana na makaburi yasiyoonekana, ambayo watu wapitao juu yake hawana habari nayo. Mtu mmoja katika wana-sheria akajibu, akamwambia, Mwalimu, kwa kusema hayo umetushutumu sisi nasi. Akasema, Nanyi wana-sheria, ole wenu, kwa sababu mwawatwika watu mizigo isiyochukulika, wala ninyi wenyewe hamwigusi mizigo hiyo hata kwa kimoja cha vidole vyenu. Ole wenu, kwa kuwa mwajenga maziara ya manabii, na baba zenu ndio waliowaua. Basi, mwashuhudia na kuziridhia kazi za baba zenu; kwa kuwa wao waliwaua nanyi mwawajengea maziara. Na kwa sababu hiyo hekima ya Mungu ilisema, Tazama, nitatuma kwao manabii na mitume, nao watawaua baadhi yao na kuwafukuza, ili kwa kizazi hiki itakwe damu ya manabii wote, iliyomwagika tangu kupigwa msingi wa ulimwengu; tangu damu ya Habili hata damu ya Zakaria, aliyeuawa kati ya madhabahu na hekalu. Naam, nawaambieni ya kwamba itatakwa kwa kizazi hiki. Ole wenu, enyi wana-sheria, kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa maarifa; wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia. Alipotoka humo, waandishi na Mafarisayo walianza kumsonga vibaya, na kumchokoza kwa maswali mengi, wakimvizia, ili wapate neno litokalo kinywani mwake.