Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yn 4:31-42

Yn 4:31-42 SUV

Huko nyuma wanafunzi wakamsihi wakisema, Rabi, ule. Akawaambia, Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi. Basi wanafunzi wake wakasemezana, Je! Mtu amemletea chakula? Yesu akawaambia, Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake. Hamsemi ninyi, Bado miezi minne, ndipo yaja mavuno? Tazama, mimi nawaambieni, Inueni macho yenu myatazame mashamba, ya kuwa yamekwisha kuwa meupe, tayari kwa mavuno. Naye avunaye hupokea mshahara, na kukusanya matunda kwa uzima wa milele, ili yeye apandaye na yeye avunaye wapate kufurahi pamoja. Kwa maana hapo neno hilo huwa kweli, Mmoja hupanda akavuna mwingine. Mimi naliwatuma myavune yale msiyoyataabikia; wengine walitaabika, nanyi mmeingia katika taabu yao. Na katika mji ule Wasamaria wengi walimwamini kwa sababu ya neno la yule mwanamke, aliyeshuhudia kwamba, Aliniambia mambo yote niliyoyatenda. Basi wale Wasamaria walipomwendea, walimsihi akae kwao; naye akakaa huko siku mbili. Watu wengi zaidi wakaamini kwa sababu ya neno lake. Wakamwambia yule mwanamke, Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu; maana sisi tumesikia wenyewe, tena twajua ya kuwa hakika huyu ndiye Mwokozi wa ulimwengu.

Soma Yn 4