Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yn 2:13-25

Yn 2:13-25 SUV

Na Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu; naye Yesu akakwea mpaka Yerusalemu. Akaona pale hekaluni watu waliokuwa wakiuza ng’ombe na kondoo na njiwa, na wenye kuvunja fedha wameketi. Akafanya kikoto cha kambaa, akawatoa wote katika hekalu, na kondoo na ng’ombe; akamwaga fedha za wenye kuvunja fedha, akazipindua meza zao; akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoeni haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara. Wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa imeandikwa, Wivu wa nyumba yako utanila. Basi Wayahudi wakajibu, wakamwambia, Ni ishara gani utuonyeshayo, kwamba unafanya haya? Yesu akajibu, akawaambia, Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha. Basi Wayahudi wakasema, Hekalu hili lilijengwa katika muda wa miaka arobaini na sita, nawe utalisimamisha katika siku tatu? Lakini yeye alinena habari za hekalu la mwili wake. Basi alipofufuka katika wafu, wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa alisema hivi, wakaliamini lile andiko na lile neno alilolinena Yesu. Hata alipokuwapo Yerusalemu kwenye sikukuu wakati wa Pasaka, watu wengi waliamini jina lake, walipoziona ishara zake alizozifanya. Lakini Yesu hakujiaminisha kwao; kwa kuwa yeye aliwajua wote; na kwa sababu hakuwa na haja ya mtu kushuhudia habari za mwanadamu; kwa maana yeye mwenyewe alijua yaliyomo ndani ya mwanadamu.

Soma Yn 2

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha