Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yer 18:1-12

Yer 18:1-12 SUV

Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, kusema, Ondoka, ukashuke mpaka nyumba ya mfinyanzi, na huko nitakusikizisha maneno yangu. Basi nikashuka mpaka nyumba ya mfinyanzi, na tazama, alikuwa akifanya kazi yake kwa magurudumu. Na chombo kile, alichokuwa akikifinyanga, kilipoharibika mkononi mwake yule mfinyanzi, alikifanyiza tena kuwa chombo kingine, kama alivyoona vema yule mfinyanzi kukifanya. Ndipo neno la BWANA likanijia, kusema, Ee nyumba ya Israeli, je! Siwezi mimi kuwatendea ninyi vile vile kama mfinyanzi huyu alivyotenda? Asema BWANA. Angalieni, kama udongo ulivyo katika mkono wa mfinyanzi, ndivyo mlivyo ninyi katika mkono wangu, Ee nyumba ya Israeli. Wakati wo wote nitakapotoa habari za taifa, na habari za ufalme, kuung’oa, na kuuvunja, na kuuangamiza; ikiwa taifa lile nililolitaja litageuka, na kuacha maovu yake nitaghairi, nisitende mabaya yale niliyoazimia kuwatenda. Na wakati wo wote nitakapotoa habari za taifa, na habari za ufalme, kuujenga na kuupanda, ikiwa watatenda maovu mbele za macho yangu, wasiitii sauti yangu, basi nitaghairi, nisitende mema yale niliyoazimia kuwatendea. Haya! Basi, ukawaambie watu wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu, ukisema, BWANA asema hivi, Tazama, ninafinyanga mabaya juu yenu, na kuwaza mawazo juu yenu; rudini sasa, kila mmoja na aiache njia yake mbaya; zitengenezeni njia zenu, na matendo yenu. Lakini wao wasema, Hapana tumaini lo lote; maana sisi tutafuata mawazo yetu wenyewe, nasi tutatenda kila mmoja wetu kwa kuufuata ushupavu wa moyo wake mbaya.

Soma Yer 18