Yer 15:1-9
Yer 15:1-9 SUV
Ndipo BWANA akaniambia, Hata wangesimama mbele zangu Musa na Samweli, moyo wangu usingewaelekea watu hawa; watupe, watoke mbele za macho yangu, wakaende zao. Kisha itakuwa, hapo watakapokuambia, Tutoke, tuende wapi? Utawaambia, BWANA asema hivi, Walioandikiwa kufa, watakwenda kufa; au kufa kwa upanga, watakufa kwa upanga; au kufa kwa njaa, watakufa kwa njaa, au kutekwa nyara, watakuwa mateka. Nami nitaamrisha juu yao namna nne, asema BWANA; upanga uue, na mbwa wararue, na ndege wa angani, na wanyama wakali wa nchi, wale na kuangamiza. Nami nitawafanya kuwa kitu cha kutisha katika falme zote za duniani, kwa sababu ya Manase, mwana wa Hezekia mfalme wa Yuda, kwa sababu ya mambo aliyoyatenda katika Yerusalemu. Maana ni nani atakayekuhurumia, Ee Yerusalemu? Au ni nani atakayekulilia? Au ni nani atakayegeuka upande ili kuuliza habari za hali yako? Umenikataa mimi, asema BWANA, umerudi nyuma; ndiyo maana nimenyosha mkono wangu juu yako, na kukuangamiza; nimechoka kwa kughairi. Nami nimewapepea kwa kipepeo katika malango ya nchi nimewaondolea watoto wao, nimewaharibu watu wangu; hata hivyo hawakurudi na kuziacha njia zao. Wajane wao wameongezeka kwangu kuliko mchanga wa bahari; nimeleta mwenye kuteka wakati wa adhuhuri juu ya mama wa vijana; nimeleta hamu na maogofyo yampate ghafula. Mwanamke aliyezaa watoto saba anazimia; ametoa roho; jua lake limekuchwa, ungali ni wakati wa mchana; ametahayarika na kufedheheka; na mabaki yao nitawatoa kwa upanga mbele ya adui zao, asema BWANA.