Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Amu 16:4-22

Amu 16:4-22 SUV

Ikawa baada ya hayo akampenda mwanamke mmoja katika bonde la Soreki, jina lake akiitwa Delila. Nao wakuu wa Wafilisti wakamwendea, wakamwambia, Mbembeleze, upate kujua asili ya nguvu zake nyingi, na jinsi tutakavyoweza kumshinda, tupate kumfunga na kumtesa; nasi tutakupa kila mtu fedha elfu na mia moja. Delila akamwambia Samsoni, Tafadhali uniambie asili ya nguvu zako nyingi, na jinsi uwezavyo kufungwa, ili uteswe. Samsoni akamwambia, Wakinifunga kwa kamba mbichi saba ambazo hazijakauka bado, hapo ndipo nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu. Ndipo wakuu wa Wafilisti wakamletea kamba mbichi saba zisizokauka, naye akamfunga nazo. Na yule mwanamke alikuwa na watu katika chumba cha ndani, wakimwotea. Basi akamwambia Samsoni, Wafilisti wanakujia. Ndipo akazikata zile kamba kama vile uzi wa pamba ukatwavyo ukiguswa na moto. Basi hiyo asili ya nguvu zake haikujulikana. Delila akamwambia Samsoni, Tazama, umenidhihaki, na kuniambia uongo; sasa tafadhali, niambie, waweza kufungwa kwa kitu gani? Akamwambia Wakinifunga tu kwa kamba mpya ambazo mtu hakufanya kazi nazo, hapo ndipo nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu. Basi Delila akatwaa kamba mpya akamfunga nazo, akamwambia, Wafilisti wanakujia, Samsoni. Na wale wenye kuotea walikuwa katika chumba cha ndani. Naye akazikata, akazitupa kutoka mikononi mwake kama uzi. Delila akamwambia Samsoni, Hata sasa umenidhihaki, umeniambia maneno ya uongo; niambie sasa, waweza kufungwa kwa kitu gani? Akamwambia, Ukivifuma hivi vishungi saba vya nywele za kichwa changu katika mtande wa nguo. Basi akazifunga kwa msumari, akamwambia Samsoni, Wafilisti wanakujia. Naye akaamka usingizini, akaung’oa ule msumari, na ule mtande. Mwanamke akamwambia, Wawezaje kusema, Nakupenda; na moyo wako haupo pamoja nami? Umenidhihaki mara hizi tatu, wala hukuniambia asili ya nguvu zako nyingi. Ikawa, kwa vile alivyomsumbua kwa maneno yake kila siku, na kumwudhi, roho yake ikadhikika hata kufa. Ndipo alipomwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akamwambia, Wembe haukupita juu ya kichwa changu kamwe; maana mimi nimekuwa Mnadhiri wa Mungu, tangu tumboni mwa mama yangu; nikinyolewa, ndipo nguvu zangu zitanitoka, nami nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu. Delila alipoona ya kuwa amemwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akatuma mtu akawaita wakuu wa Wafilisti, akisema, Njoni huku mara hii tu, maana ameniambia yote aliyo nayo moyoni mwake. Ndipo wakuu wa Wafilisti wakamwendea wakachukua ile fedha mikononi mwao. Naye akamlaza usingizi magotini pake. Kisha akamwita mtu akavinyoa vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake; akaanza kumsumbua, nguvu zake zikamtoka. Kisha akasema, Samsoni, Wafilisti wanakujia. Akaamka katika usingizi wake, akasema, Nitakwenda nje kama siku nyingine, na kujinyosha. Lakini hakujua ya kuwa BWANA amemwacha. Wafilisti wakamkamata, wakamng’oa macho; wakatelemka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba; naye alikuwa akisaga ngano katika gereza. Lakini zile nywele za kichwa chake zikaanza kukua tena baada ya kunyolewa kwake.

Soma Amu 16