Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isa 44:9-20

Isa 44:9-20 SUV

Wachongao sanamu, wote ni ubatili; wala mambo yao yawapendezayo hayatafaa kitu; wala mashahidi wao wenyewe hawaoni, wala hawajui; ili watahayarike. Ni nani aliyejichongea mungu mmoja, au aliyesubu sanamu isiyofaa kitu? Tazama, wenziwe wote watatahayari; na mafundi, hao ni wanadamu; na wakusanyike pamoja, wakasimame; wataogopa na kutahayari pamoja. Mfua chuma hufanza shoka, hufanya kazi kwa makaa, huitengeneza sanamu kwa nyundo, huifanyiza kwa nguvu za mkono wake; naam, huona njaa, nguvu zake zikampungukia; asipokunywa maji huzimia. Seremala hunyosha uzi; huiandika kwa kalamu ya mate; huitengeneza kwa randa, huiandika kwa bikari, huifanza kwa mfano wa mwanadamu, sawasawa na uzuri wa mwanadamu, ili ikae nyumbani. Yeye hujikatia mierezi, hutwaa mtiriza, na mwaloni, hujichagulia mti mmoja katika miti ya msituni; hupanda mvinje, mvua ikausitawisha. Kisha utamfaa mwanadamu kwa kuni; hutwaa kipande, akaota moto; naam, huuwasha moto, akaoka mkate; naam, huufanya mungu, akauabudu; huifanya sanamu ya kuchonga, akaisujudia. Sehemu moja huiteketeza; kwa sehemu nyingine hula nyama; huoka chakula kiokwacho, akashiba; naam, huota moto, akasema, Aha, nimeota moto, nimeona moto; na kwa sehemu iliyobakia hufanya mungu, yaani, sanamu yake ya kuchonga; husujudu mbele yake akaiabudu, akaiomba, akasema, Uniokoe; maana wewe u mungu wangu. Hawajui wala hawafikiri; maana amewafumba macho, wasione, na mioyo yao, wasiweze kufahamu. Wala hapana atiaye moyoni, wala hapana maarifa, wala fahamu kusema, Nimeteketeza sehemu motoni, naam, pia nimeoka mkate juu ya makaa yake; nimeoka nyama nikaila; nami, je! Kilichobaki nikifanye kuwa chukizo? Je! Nisujudie shina la mti? Hula majivu; moyo uliodanganyika umempotosha, asiweze kuiokoa nafsi yake, wala kusema, Je! Sio uongo mkononi mwangu?

Soma Isa 44