Isa 38:1-8
Isa 38:1-8 SUV
Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, BWANA asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona. Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba BWANA, akasema, Ee BWANA, kumbuka haya, nakusihi, kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana. Ikawa, neno la BWANA likamjia Isaya, kusema, Enenda ukamwambie Hezekia, BWANA, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano. Nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu. Jambo hili liwe ishara kwako, itokayo kwa BWANA, ya kuwa BWANA atalitimiza jambo hili alilolisema; Tazama, nitakirudisha nyuma kivuli madaraja kumi, ambayo kilishuka juu ya duara ya Ahazi kwa sababu ya jua. Basi jua likarudi madaraja kumi katika hiyo duara, ambayo limekwisha kushuka.