Isaya 38:1-8
Isaya 38:1-8 NENO
Katika siku hizo Hezekia akaugua, naye akawa karibu kufa. Nabii Isaya mwana wa Amozi akaenda kwake na kumwambia, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Tengeneza mambo ya nyumba yako, kwa sababu utakufa, hutapona.” Hezekia akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Mwenyezi Mungu: “Ee Mwenyezi Mungu, kumbuka jinsi nilivyoenenda mbele zako kwa uaminifu na kujitoa kwa moyo wangu wote, na kufanya yaliyo mema machoni pako.” Naye Hezekia akalia kwa uchungu. Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likamjia Isaya, kusema: “Nenda ukamwambie Hezekia, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba yako Daudi: Nimeyasikia maombi yako na nimeona machozi yako. Nitakuongezea miaka kumi na tano katika maisha yako. Nami nitakuokoa wewe pamoja na mji huu kutoka mkononi mwa mfalme wa Ashuru. Nitaulinda mji huu. “ ‘Hii ndiyo ishara ya Mwenyezi Mungu kwako kwamba Mwenyezi Mungu atafanya kile alichoahidi: Nitafanya kivuli cha jua kwenye ngazi iliyojengwa na Ahazi kirudi nyuma madaraja kumi.’ ” Hivyo jua likarudi nyuma madaraja kumi ambayo lilikuwa limeshuka.