Hag UTANGULIZI
UTANGULIZI
Kitabu hiki kinaitwa cha Hagai, mmojawapo wa manabii wa kwanza kabisa kutoa unabii Yerusalemu baada ya Wayahudi kutoka uhamishoni Babeli. Nabii Hagai alifanya kazi na Nabii Zekaria karibu mwaka 520 Kabla ya Kristo Kuzaliwa. Maana ya jina Hagai ni “Furaha.”
Wayahudi walipotoka uhamishoni wakiongozwa na Zerubabeli mjukuu wa mfalme Yehoyakini na kuhani mkuu Yoshua walikuwa na hamasa kidini na kisiasa. Madhabahu ilijengwa kwa muda mfupi sana na msingi wa Hekalu ukawekwa. Hata hivyo, walikatishwa tamaa na watu fulani waliopinga ujenzi huo. Kwa muda wa miaka kumi na sita kazi ya ujenzi wa Hekalu ilikuwa imesitishwa.
Mungu alimtuma Hagai kutoa ujumbe kwa Wayahudi. Mara nne alitoa ujumbe kwa kuonya, kuhamisha na kutia moyo ujenzi wa Hekalu (1:1-15; 2:1-23). Jambo kuu la ujumbe huu sio kujenga Hekalu bali Mungu kuwa na umuhimu wa kwanza katika maisha yao na kwa kuwa na uhusiano mwema naye. Wayahudi walitumia visingizio vya waliowapinga, hali mbaya ya uchumi, na ugumu wa maisha kuwa udhuru wa kutotoa muhimu wa kwanza kwa Mungu na kutoendelea na ujenzi wa Hekalu. Lakini wakati huo huo walijishughulisha na ujenzi wa nyumba zao, na kufanya sherehe mbalimbali. Kwa kuwa walijiweka mbele walitumia vifaa vya ujenzi vyenye thamani kubwa kujenga nyumba zao wenyewe badala ya Nyumba ya Mungu.
Hagai anaonya kwa kusema kuwa hawana budi kujisahihisha kwa kuacha ubinafsi na unajisi. Uasi na unajisi huleta hukumu. Utii, kujitoa na kumtegemea Mungu huwa na baraka. Watu waliitikia kwa toba. Baada ya majuma matatu walianza kazi ya ujenzi wa Hekalu. Hagai alisema kwamba kazi yao inaweka msingi wa taifa ambalo baadaye litaongozwa na Masihi. Hagai alimtia moyo Zerubabeli kuwa ni mjumbe mteule wa Mungu, na katika yeye ahadi za Mungu kwa nyumba ya Daudi zitatimizwa.
Yaliyomo:
1. Agizo na utekelezaji wa kujenga upya hekalu, Sura 1:1-15
2. Utukufu wa Hekalu litakalojengwa, Sura 2:1-9
3. Unajisi na ahadi za baraka, Sura 2:10-19
4. Ahadi ya Mungu kwa Zerubabeli, Sura 2:20-23
Iliyochaguliwa sasa
Hag UTANGULIZI: SUV
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.