Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Eze UTANGULIZI

UTANGULIZI
Ezekieli mwana wa Buzi alikuwa mwenyeji wa Yerusalemu. Maana ya jina lake ni “Mungu hunitia nguvu”. Alikuwa ameoa, mkewe alikufa wakati wa kuzingirwa kwa Yerusalemu mwaka 587 Kabla ya Kristo Kuzaliwa (24:15-24). Ezekieli ni mmoja wa vijana waliokuwa makuhani, mwenye elimu, usanii wa vyombo vinavyosafiri majini (27:1-9) na ujuzi wa historia (16:3). Watu walimwendea kupata ushauri. Alikuwa na nyumba yake (8:1).
Wababeli walipotawala Yuda, mwanzoni walimruhusu mfalme wa Yuda aendelee kuongoza nchi yake lakini atii mtawala wa Babeli na kumtolea kodi kubwa. Vile vile, baadhi ya vijana wa Kiyahudi wenye ujuzi na uwezo katika ukoo wa kifalme na familia za wakuu nchini walipelekwa uhamishoni Babeli (2 Fal 24:1a). Mfalme wa Yuda alipoasi mwaka 597 K.K. yeye pamoja na watu wake mashauri walichukuliwa nchini Babeli (2 Nya 36:9:10). Ezekieli alikuwa kati ya vijana waliochukuliwa kwenye awamu ya pili pamoja na mfalme wa Yuda.
Ezekieli aliitwa kuwa nabii baada ya kuishi miaka mitano huko Babeli. Aliendelea kuhubiri kwa muda unaozidi miaka ishirini na saba (29:17). Miaka thelathini inayotajwa (1:1) huenda ikawa ni umri wake. Mahubiri yake yaliwalenga waliobaki Yerusalemu na Yuda pia waliokuwa uhamishoni. Vile vile aligusia mataifa yaabuduyo sanamu na kutendea Israeli jeuri na ukatili. Nabii Ezekieli anajiita “mlinzi” na “mwonyaji” ili watu watubu na kuacha uovu wao (33:7-9). Nabii alipata ushupavu na nguvu za kuhubiri baada ya kupewa agizo kutoka kwa Mungu (11:4-5) na kuonyeshwa maono juu ya enzi na utukufu wa Mungu (11:22-25; Sura 1, 10 na 3:23).
Nabii Ezekieli anasema kuwa Hekalu limenajisiwa kwa ibada za sanamu na mizimu (5:11; 20:24; 8:5-13) pamoja na hata kutoa watoto kafara (16:20-21). Makuhani wameshindwa wajibu wao na viongozi hawana adili (22:23-30). Ijapokuwa watu walijua lililo jema hawakulitenda ila walifanya kinyume chake (5:6-8; 18:5-8; 33:25-30). Kwa kuwa taifa limeasi, Mungu amewaacha (11:22-23). Nabii aliwaonya na kuwatahadharisha watu juu ya hukumu ya Mungu. Adui wa Yuda watakuwa chombo cha kuadhibu taifa la Agano (21:18-23; 24:1-4). Yerusalemu utabomolewa na wakazi watapelekwa uhamishoni Babeli. Hukumu ni kwa kila anayeasi. Baadhi ya Wayahudi walisingizia kuwa mababu zao ndio wanaosababisha hukumu hiyo. Hata hivyo, nabii Ezekieli analikataa wazo hilo na kusema kuwa kila mtu anahukumiwa kwa ajili ya makosa yake mwenyewe (18:1-32). Mtu harithishwi uchaji na utakatifu wa Mungu (14:20), hivyo wageuze nia na matendo yao, maana wakiendelea kuasi wataadhibiwa (33:11). Ujumbe wa hukumu ulitolewa kwa mataifa jirani wa Israeli pia.
Ezekieli alitoa ujumbe wa kutumainisha siku ambapo Mungu wao atarudisha Israeli na Yuda katika nchi yao. Watu wataacha dhambi zao, Mungu atatia roho mpya na moyo mpya ndani yao (11:19-20; 36:25-26). Taifa lililoonekana kuwa mfu litahuishwa liwe hai (Sura 37). Masihi aitwaye Daudi ataangamiza adui wao na kuongoza watu wake nao watafuata amri zake (34:23-24).
Watajenga hekalu jipya lenye “utukufu wa BWANA” katika Yerusalemu (40:1-16; 43:1-5). Ujumbe wa Ezekieli ni wa hukumu, tulizo, matumaini, kufanywa upya na utakatifu wa Mungu. Ujumbe umewafikia walengwa kwa njia ya hadithi, mifano, ishara na maigizo.
Yaliyomo:
1. Wito wa Ezekieli, Sura 1–3
2. Hukumu kwa Yerusalemu, Sura 4–7
3. Dhambi za Yerusalemu, Sura 8–24
4. Hukumu kwa mataifa saba ya kigeni, Sura 25–32
5. Unabii kuhusu kurudi nchini Israeli na adhabu kwa adui, Sura 33–39

Iliyochaguliwa sasa

Eze UTANGULIZI: SUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia