Eze 44:15-29
Eze 44:15-29 SUV
Lakini makuhani Walawi, wana wa Sadoki, waliolinda ulinzi wa patakatifu pangu, hapo wana wa Israeli walipopotea na kuniacha, hao ndio watakaonikaribia ili kunihudumia; nao watasimama mbele zangu, kunitolea mafuta na damu, asema Bwana MUNGU; wataingia patakatifu pangu, nao wataikaribia meza yangu, ili kunihudumia, nao watalinda ulinzi wangu. Itakuwa, hapo watakapoingia kwa malango ya ua wa ndani, watavikwa mavazi ya kitani; wala sufu haitakuwa juu yao, maadamu wanahudumu katika malango ya ua wa ndani, na ndani ya nyumba. Watakuwa na vilemba vya kitani juu ya vichwa vyao, nao watakuwa na suruali za kitani viunoni mwao; hawatajifunga kiunoni kitu cho chote kifanyacho jasho. Nao watakapotoka kuingia ua wa nje, yaani, ua wa nje wa watu, ndipo watakapoyavua mavazi yao waliyovaa katika huduma yao, na kuyaweka katika vile vyumba vitakatifu, nao watavaa mavazi mengine, wasije wakawatakasa watu kwa mavazi yao. Hawatanyoa vichwa vyao, wala hawataacha nywele zao kuwa ndefu sana; watazipunguza nywele za vichwa vyao tu. Wala kuhani awaye yote hatakunywa mvinyo, aingiapo katika ua wa ndani. Wala hawataoa wanawake wajane, wala mwanamke aliyeachwa na mume wake; lakini watatwaa mabikira wa wazao wa nyumba ya Israeli, au mjane aliyefiwa na mumewe kuhani. Nao watawafundisha watu wangu tofauti iliyopo kati ya vitu vitakatifu na vitu vya sikuzote, na kuwafundisha kupambanua kati ya yaliyo machafu na yaliyo safi. Na katika mashindano watasimama ili kuamua; wataamua sawasawa na hukumu zangu; nao watazishika sheria zangu, na amri zangu, katika sikukuu zangu zote zilizoamriwa; nao watazitakasa sabato zangu. Wala hawatakaribia maiti na kujitia unajisi; ila kwa ajili ya baba, au mama, au mwana, au binti, au ndugu mwanamume, au ndugu mwanamke asiyeolewa bado, waweza kujitia unajisi. Naye akiisha kutakaswa watamhesabia siku saba. Na katika siku atakayoingia ndani ya patakatifu, katika ua wa ndani, ili kuhudumu ndani ya patakatifu, atatoa sadaka yake ya dhambi, asema Bwana MUNGU. Nao watakuwa na urithi; mimi ni urithi wao; wala hamtawapa milki iwayo yote katika Israeli; mimi ni milki yao. Wataila sadaka ya unga, na sadaka ya dhambi, na sadaka ya hatia, na kila kitu katika Israeli kilichowekwa wakfu kitakuwa chao.