Kut 23:20-33
Kut 23:20-33 SUV
Tazama, mimi namtuma malaika aende mbele yako, ili akulinde njiani na kukupeleka mpaka mahali pale nilipokutengezea. Jitunzeni mbele yake, mwisikize sauti yake; wala msimtie kasirani; maana, hatawasamehe makosa yenu; kwa kuwa jina langu limo ndani yake. Lakini ukiisikiza sauti yake kweli, na kuyatenda yote ninenayo mimi; ndipo mimi nitakuwa ni adui wa adui zako, na mtesi wa hao wakutesao. Kwa kuwa malaika wangu atatangulia mbele yako, na kukufikisha kwenye Mwamori, na Mhiti, na Mperizi, na Mkanaani, na Mhivi, na Myebusi; nami nitawakatilia mbali. Usiisujudie miungu yao, wala kuitumikia; wala usitende mfano wa matendo yao; bali utaiangamiza kabisa, na nguzo zao utazivunja vipande vipande. Nanyi mtamtumikia BWANA, Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea ugonjwa kati yako. Hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba, wala aliye tasa, katika nchi yako; na hesabu ya siku zako nitaitimiza. Nitatuma utisho wangu utangulie mbele yako, nami nitawafadhaisha watu wote utakaowafikilia, nami nitawafanya hao adui zako wote wakuonyeshe maungo yao. Nami nitapeleka mavu mbele yako, watakaomfukuza Mhivi, na Mkanaani, na Mhiti, watoke mbele yako. Sitawafukuza mbele yako katika mwaka mmoja; nchi isiwe ukiwa, na wanyama wa bara wakaongezeka kukusumbua. Nitawafukuza kidogo kidogo mbele yako, hata utakapoongezeka wewe, na kuirithi hiyo nchi. Nami nitakuwekea mpaka wako tangu Bahari ya Shamu hata bahari ya Wafilisti, tena tangu jangwani hata huo Mto; kwa kuwa nitawatia wenyeji wa nchi mkononi mwako; nawe utawafukuza mbele yako. Usifanye maagano pamoja nao, wala pamoja na miungu yao. Wasikae katika nchi yako, wasije wakakufanya kunitendea mimi dhambi; kwa sababu ukiitumikia miungu yao, jambo hili halikosi litakuwa ni tanzi kwako.