Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Est 4:5-16

Est 4:5-16 SUV

Kisha Esta akamwita Hathaki, msimamizi-wa-nyumba mmojawapo wa mfalme, aliyemwagiza amhudumu Esta, akamtuma kwa Mordekai, ili ajue mambo hayo, na maana yake ni nini. Basi yule Hathaki akatoka nje kumwendea Mordekai kwenye uwanda wa mji ulipo mbele ya mlango wa mfalme. Naye Mordekai akamweleza yote yaliyompata, na hesabu ya fedha Hamani aliyoahidi kulipa katika hazina ya mfalme, ili Wayahudi waangamizwe. Pia akampa na nakili ya andiko la mbiu ya kuwaangamiza, iliyotangazwa Shushani, ili amwonyeshe Esta, na kumweleza; tena amwagize aingie kwa mfalme, kumsihi na kuwaombea watu wake. Basi Hathaki akaja, akamwambia Esta maneno ya Mordekai. Ndipo Esta akasema na Hathaki, akamtuma tena kwa Mordekai, kusema, Watumwa wote wa mfalme wanajua sana, hata na watu wa majimbo ya mfalme, ya kwamba mtu ye yote, akiwa mwanamume au mwanamke, atakayemjia mfalme katika ua wa ndani, wala hakuitwa, kuna sheria moja kwake, ni kwamba auawe; isipokuwa yeye ambaye mfalme atamnyoshea fimbo ya dhahabu, ili aishi; wala mimi sikuitwa niingie kwa mfalme yapata siku thelathini. Basi wakamwambia Mordekai maneno ya Esta. Naye Mordekai akawaagiza wampelekee Esta jibu la kusema, Wewe usijidhanie kuwa wewe utaokoka nyumbani mwa mfalme, zaidi ya Wayahudi wote. Kwa maana wewe ukinyamaza kabisa wakati huu, ndipo kutakapowatokea Wayahudi msaada na wokovu kwa njia nyingine; ila wewe utaangamia pamoja na mlango wote wa baba yako; walakini ni nani ajuaye kama wewe hukuujia ufalme kwa ajili ya wakati kama huo? Basi Esta akawatuma ili wamjibu Mordekai, Uende ukawakusanye Wayahudi wote waliopo hapa Shushani, mkafunge kwa ajili yangu; msile wala kunywa muda wa siku tatu, usiku wala mchana, nami na wajakazi wangu tutafunga vile vile; kisha nitaingia kwa mfalme, kinyume cha sheria; nami nikiangamia, na niangamie.

Soma Est 4

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Est 4:5-16