Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kum 28:58-68

Kum 28:58-68 SUV

Kama hutaki kutunza kufanya maneno yote ya torati hii yaliyoandikwa katika kitabu hiki, upate kulicha jina hili la fahari na utisho, BWANA, MUNGU WAKO; ndipo atakapofanya BWANA mapigo yako yawe ya ajabu, na mapigo ya uzao wako, mapigo makubwa kwa kweli, ya kudumu sana, na magonjwa mazito ya kudumu sana. Naye atakurejezea maradhi yote ya Misri juu yako uliyokuwa ukiyaogopa, nayo yataambatana nawe. Tena kila ugonjwa, na kila pigo yasiyoandikwa katika kitabu cha torati hii, atakutia nayo BWANA juu yako, hata utakapokwisha kuangamizwa. Nanyi mtasalia wachache kwa hesabu, ninyi mliokuwa mfano wa nyota za mbinguni kwa wingi; kwa kuwa hukuisikiza sauti ya BWANA, Mungu wako. Tena itakuwa, kama vile alivyokuwa akifurahi BWANA juu yenu kwa kuwatendea mema na kuwafanya kuwa wengi, ndivyo atakavyofurahi BWANA juu yenu kwa kuwapoteza na kuwaangamiza; nanyi mtanyakuliwa katika hiyo nchi mwingiayo kuimiliki. BWANA atakutawanya katika mataifa yote, tokea ncha hii ya dunia hata ncha hii ya dunia; nawe huko utatumikia miungu mingine usiyoijua wewe wala baba zako, nayo ni miti na mawe. Wala katika mataifa hayo hutapata raha iwayo yote, wala hutakuwa na kituo cha wayo wa mguu wako; lakini BWANA atakupa huko moyo wa kutetema, na macho ya kuzimia, na roho ya kudhoofika; na uzima wako utakuwa na wasiwasi mbele yako; nawe utakuwa na woga usiku na mchana, wala hutaamini kamwe maisha yako; asubuhi utasema, Laiti ingekuwa jioni! Na jioni utasema, Laiti ingekuwa asubuhi! Kwa kicho cha moyo wako utakavyokucha, na kuona kwa macho yako utakavyoona. BWANA atakurudisha tena Misri kwa merikebu, kwa njia ambayo nilikuambia, Hutaiona tena po pote; nanyi huko mtajiuza nafsi zenu kwa adui zenu kuwa watumwa na wajakazi, wala hapana atakayewanunua.