2 Sam 3:1-11
2 Sam 3:1-11 SUV
Basi kulikuwa na vita siku nyingi kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi; Daudi akaendelea akasitawi, lakini nyumba ya Sauli ikaendelea kudhoofika. Naye Daudi akazaliwa wana huko Hebroni; mzaliwa wake wa kwanza alikuwa Amnoni, wa Ahinoamu wa Yezreeli; na wa pili wake Danieli, wa Abigaili mkewe Nabali wa Karmeli; na wa tatu Absalomu, mwana wa Maaka binti Talmai, mfalme wa Geshuri, na wa nne Adoniya, mwana wa Hagithi; na wa tano Shefatia, mwana wa Abitali; na wa sita Ithreamu, wa Egla, mkewe Daudi. Hawa walizaliwa kwa Daudi huko Hebroni. Ikawa, wakati vilipokuwapo vita kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi, Abneri akajipatia nguvu nyumbani kwa Sauli. Basi Sauli alikuwa na suria, jina lake akiitwa Rispa, binti Aya; Ishboshethi akamwuliza Abneri, Kwa nini umeingia kwa suria ya babangu? Basi Abneri akakasirika kwa maneno ya Ishboshethi, akasema, Je! Mimi ni kichwa cha mbwa, aliye wa Yuda? Hata leo hivi nawafanyia fadhili nyumba ya Sauli babako, na ndugu zake, na rafiki zake, nisikutie wewe mkononi mwa Daudi; nawe hata hivyo wanitia hatiani leo kwa mwanamke huyu. Mungu amfanyie Abneri vivyo, na kuzidi, nisipomtendea Daudi kama vile BWANA alivyomwapia; kuupitisha ufalme toka nyumba ya Sauli, na kukisimamisha kiti cha Daudi juu ya Israeli, na juu ya Yuda, toka Dani mpaka Beer-sheba. Wala hakuweza kumjibu Abneri tena, kwa sababu alimwogopa.