2 Samweli 3:1-11
2 Samweli 3:1-11 NEN
Vita kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi vilidumu kwa muda mrefu. Daudi akaendelea kuwa imara zaidi na zaidi, wakati nyumba ya Sauli iliendelea kudhoofika zaidi na zaidi. Wana walizaliwa kwa Daudi huko Hebroni: Mzaliwa wake wa kwanza alikuwa Amnoni mwana wa Ahinoamu wa Yezreeli; mzaliwa wake wa pili alikuwa Danieli mwana wa Abigaili, mjane wa Nabali wa Karmeli; wa tatu, Absalomu mwana wa Maaka, binti Talmai mfalme wa Geshuri; wa nne, Adoniya mwana wa Hagithi; wa tano, Shefatia mwana wa Abitali; wa sita, Ithreamu mwana wa Egla, mkewe Daudi. Hawa ndio waliozaliwa kwa Daudi huko Hebroni. Wakati wa vita kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi, Abneri alikuwa anajiimarisha katika nafasi yake kwenye nyumba ya Sauli. Basi Sauli alikuwa amekuwa na suria, jina lake Rispa binti wa Aiya. Naye Ish-Boshethi akamwambia Abneri, “Kwa nini umekutana kimwili na suria wa baba yangu?” Abneri akakasirika sana kwa sababu ya kile Ish-Boshethi alichosema, naye akamjibu, “Je, mimi ni kichwa cha mbwa, kwa upande wa Yuda? Siku hii ya leo mimi ni mtiifu kwa nyumba ya baba yako Sauli, kwa jamaa yake na rafiki zake. Sijakukabidhi kwa Daudi, lakini bado unanilaumu kwa kosa la kuhusika na huyu mwanamke! Mungu na amshughulikie Abneri, tena kwa ukali, ikiwa sitafanya kwa ajili ya Daudi kile BWANA alichomwahidi kwa kiapo, na kuuhamisha ufalme kutoka kwenye nyumba ya Sauli na kuimarisha kiti cha ufalme cha Daudi juu ya Israeli na Yuda kuanzia Dani mpaka Beer-Sheba.” Ish-Boshethi hakuthubutu kusema neno jingine kwa Abneri, kwa sababu alimwogopa Abneri.