Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Sam 21:15-22

2 Sam 21:15-22 SUV

Basi kulikuwa na vita tena kati ya Wafilisti na Israeli; Daudi akashuka mpaka Gobu, na watumishi wake pamoja naye, akapigana na Wafilisti; naye Daudi akaishiwa na nguvu. Naye Ishi-benobu, aliyekuwa mmojawapo wa Warefai, ambaye uzito wa mkuki wake ulikuwa shekeli mia tatu za shaba kwa uzani, naye amejifungia upanga mpya, alijaribu kumwua Daudi. Lakini Abishai, mwana wa Seruya, akamsaidia, akampiga Mfilisti, akamwua. Ndipo watu wa Daudi wakamwapia, wakasema, Wewe hutatoka tena pamoja nasi kwenda vitani, usije ukaizima taa ya Israeli. Ikawa baada ya hayo, kulikuwa na vita tena na Wafilisti huko Gobu; ndipo Sibekai, Mhushathi, alipomwua Safu, aliyekuwa mmojawapo wa Warefai. Kulikuwa na vita tena na Wafilisti huko Gobu; na Elhanani, mwana wa Yairi, Mbethlehemi, alimwua Goliathi, Mgiti, ambaye mti wa mkuki wake ulikuwa kama mti wa mfumaji. Kulikuwa na vita tena huko Gathi; ambako kulikuwa na mtu mrefu sana, mwenye vidole sita katika kila mkono, na vidole sita katika kila mguu, jumla yake ishirini na vinne; yeye naye alizaliwa kwa Mrefai. Naye huyo alipowatukana Israeli, ndipo Yonathani, mwana wa Shama, nduguye Daudi, akamwua. Hao wanne walizaliwa kwake huyo Mrefai wa Gathi; wakaanguka kwa mkono wa Daudi, na kwa mikono ya watumishi wake.