2 Sam 19:1-10
2 Sam 19:1-10 SUV
Kisha Yoabu akaambiwa, Angalia, mfalme anamlilia Absalomu na kumwombolezea. Na kushinda kwao vitani siku ile kukageuzwa kuwa maombolezo kwa watu wote; maana watu walisikia siku ile ya kwamba, Mfalme anahuzunika kwa ajili ya mwanawe. Watu wakajificha siku ile, wakaingia mjini kama vile watu waonao fedheha wajifichavyo, hapo wakimbiapo vitani. Mfalme akajifunika uso; na mfalme akalia kwa sauti kuu, Mwanangu Absalomu, Absalomu, mwanangu, mwanangu! Basi Yoabu akaingia nyumbani kwa mfalme, akasema, Wewe leo umefedhehesha nyuso za watumishi wako wote, waliokuokoa leo roho yako, na roho za wanao, na za binti zako, na roho za wakezo, na roho za masuria wako; kwa kuwa unawapenda wakuchukiao, na unawachukia wakupendao. Maana umetangaza leo ya kuwa wakuu na watumishi wako si kitu kwako; maana leo nimetambua hivi; kama Absalomu angaliishi, na sisi sote tungalikufa leo, ingalikuwa vyema machoni pako. Basi sasa, ondoka, utoke nje, ukaseme na watumishi wako maneno ya kuwatuliza roho zao; maana mimi nakuapia kwa BWANA, usipotoka, hatabaki hata mtu mmoja pamoja nawe usiku huu; na mambo haya yatakuwa mabaya kwako kuliko mabaya yote yaliyokupata tokea ujana wako hata sasa. Ndipo mfalme akaondoka, akaketi langoni. Nao wote wakaambiwa ya kwamba, Angalieni, mfalme ameketi langoni; watu wote wakaenda huko mbele ya mfalme. Basi, Israeli wote walikuwa wamekimbia kila mtu hemani kwake. Wakashindana watu wote katika kabila zote za Israeli, wakisema, Mfalme alitutoa mikononi mwa adui zetu, akatuokoa mikononi mwa Wafilisti; naye sasa amekimbia kutoka nchi hii mbele ya Absalomu. Na huyo Absalomu, tuliyemtia mafuta ili awe juu yetu, amekufa vitani. Basi sasa mbona ninyi hamsemi neno lo lote juu ya kumrudisha tena mfalme?