2 Sam 13:23-39
2 Sam 13:23-39 SUV
Ikawa baada ya miaka miwili mizima, Absalomu alikuwa na wenye kukata manyoya ya kondoo huko Baal-hasori uliopo upande wa Efraimu; naye Absalomu akawaalika wana wote wa mfalme. Absalomu akamjia mfalme, akasema, Tazama sasa, mimi mtumwa wako ninao wakata manyoya ya kondoo; basi mfalme na aende, nakusihi, na watumishi wake pamoja nami mtumwa wako. Mfalme akamwambia Absalomu, Sivyo, mwanangu, tusiende sote, tusije tukakulemea. Akamsihi sana; asikubali kwenda, ila akambariki. Ndipo akasema Absalomu, Kwamba huji, nakusihi, mwache ndugu yangu Amnoni aende nasi. Mfalme akamwambia, Kwa nini aende nawe? Lakini Absalomu akamsihi sana, naye akamwacha Amnoni na wana wote wa mfalme waende naye. Kisha Absalomu akawaamuru watumishi wake, akasema, Angalieni basi, moyo wake Amnoni utakapofurahiwa kwa mvinyo; nami nitakapowaambia, Mpigeni Amnoni, ndipo mwueni, msiogope; si mimi niliyewaamuru? Iweni hodari, iweni na ujasiri. Basi watumishi wa Absalomu wakamfanyia Amnoni kama alivyoamuru Absalomu. Ndipo wakaondoka wana wote wa mfalme, wakapanda kila mtu nyumbu wake, wakakimbia. Ikawa, walipokuwa njiani, habari zikamwasilia Daudi, kusema, Absalomu amewaua wana wote wa mfalme, wala hata mmoja wao hakusalia. Ndipo mfalme akainuka, akararua nguo zake, akalala chini; nao watumishi wake wote wakasimama karibu naye, wenye nguo zao zimeraruliwa. Akajibu Yonadabu, mwana wa Shama, nduguye Daudi, akasema, Asidhani bwana wangu ya kwamba wamewaua vijana wote, wana wa mfalme; maana ndiye Amnoni peke yake aliyekufa; yakini haya yamekusudiwa kwa kinywa chake Absalomu tangu siku ile alipotenzwa nguvu umbu lake, Tamari. Basi sasa bwana wangu mfalme asilitie neno hili moyoni, kudhani ya kwamba wana wote wa mfalme wamekufa maana ni Amnoni peke yake aliyekufa. Lakini Absalomu akakimbia. Na kijana yule aliyekuwa mlinzi akainua macho yake, akaona, na tazama, kuna watu wengi wanakuja kwa njia ya upande wa kilima nyuma yake. Ndipo Yonadabu akamwambia mfalme, Tazama, wana wa mfalme wamekuja; kama mimi mtumwa wako nilivyosema, ndivyo ilivyo. Ikawa alipokwisha kusema, tazama, wana wa mfalme walikuja, nao wakapaza sauti zao wakalia; mfalme naye akalia, na watumishi wake wote, kilio kikubwa mno. Lakini Absalomu akakimbia, akamwendea Talmai, mwana wa Amihuri, mfalme wa Geshuri. Naye Daudi akamlilia mwanawe kila siku. Basi Absalomu akakimbia, akaenda Geshuri, akakaa huko muda wa miaka mitatu. Mfalme Daudi akatamani kutoka kumwendea Absalomu kwa kuwa ametulizwa kwa habari ya Amnoni, kwa maana amekufa.