Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Sam 12:1-15

2 Sam 12:1-15 SUV

Ndipo BWANA akamtuma Nathani aende kwa Daudi. Naye akamwendea, akamwambia, Palikuwa na watu wawili katika mji mmoja; mmoja wao alikuwa tajiri, wa pili maskini. Yule tajiri alikuwa na kondoo na ng’ombe wengi sana; bali yule maskini hakuwa na kitu, ila mwana kondoo mmoja, mdogo, ambaye amemnunua na kumlea; naye akakua pamoja naye, na pamoja na wanawe; hula sehemu ya posho lake, na kukinywea kikombe chake, na kulala kifuani mwake, akawa kwake kama binti. Hata msafiri mmoja akamfikilia yule tajiri, naye akaacha kutwaa mmoja wa kondoo zake mwenyewe au mmoja wa ng’ombe zake mwenyewe, ili kumwandalia yule msafiri aliyemfikilia, bali alimnyang’anya yule maskini mwana-kondoo wake, akamwandalia yule mtu aliyemfikilia. Ndipo hasira ya Daudi ikawaka sana juu ya mtu yule; akamwambia Nathani, Aishivyo BWANA, mtu huyo aliyetenda jambo hili, hakika yake astahili kufa; naye atamrudishia yule mwana-kondoo mara nne, kwa sababu ametenda neno hili, na kwa sababu hakuwa na huruma. Basi Nathani akamwambia Daudi, Wewe ndiwe mtu huyo. BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nalikutia mafuta, uwe mfalme juu ya Israeli, nikakuokoa na mkono wa Sauli; nami nikakupa nyumba ya bwana wako, na wake za bwana wako kifuani mwako; nikakupa nyumba ya Israeli na ya Yuda; na kama hayo yangalikuwa machache, ningalikuongezea mambo kadha wa kadha. Kwa nini umelidharau neno la BWANA, na kufanya yaliyo mabaya machoni pake? Umempiga Uria, Mhiti, kwa upanga, nawe umemtwaa mkewe awe mke wako, nawe umemwua huyo kwa upanga wa wana wa Amoni. Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako. BWANA asema hivi, Angalia, nitakuondokeshea uovu katika nyumba yako, nami nitawatwaa wake zako mbele ya macho yako, na kumpa jirani yako, naye atalala na wake zako mbele ya jua hili. Maana wewe ulifanya jambo lile kwa siri; bali mimi nitalifanya jambo hili mbele ya Israeli wote na mbele ya jua. Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia BWANA dhambi. Nathani akamwambia Daudi, BWANA naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa. Lakini, kwa kuwa kwa tendo hili umewapa adui za BWANA nafasi kubwa ya kukufuru, mtoto atakayezaliwa kwako hakika yake atakufa. Naye Nathani akaondoka kwenda nyumbani kwake.

Soma 2 Sam 12

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 2 Sam 12:1-15