2 Sam 1:1-16
2 Sam 1:1-16 SUV
Ikawa baada ya kufa kwake Sauli, hapo Daudi aliporudi katika kuwaua Waamaleki, naye Daudi amekaa siku mbili katika Siklagi; hata siku ya tatu ikawa, tazama! Akaja mtu kutoka kambi ya Sauli, nguo zake zimeraruliwa, tena ana mavumbi kichwani mwake; basi, ikawa alipomfikia Daudi, akaanguka chini, akamsujudia. Daudi akamwambia, Umetoka wapi? Akamwambia, Nimeokoka katika kambi ya Israeli. Daudi akamwambia, Yalikwendaje? Tafadhali uniambie. Akajibu, Watu wamekimbia vitani, tena watu wengi wameanguka wamekufa; hata Sauli naye na Yonathani, mwanawe, wamekufa. Daudi akamwambia yule kijana aliyempa habari, Umejuaje ya kuwa Sauli na Yonathani mwanawe wamekufa? Yule kijana aliyempa habari akasema, Nalikuwapo kwa nasibu juu ya kilima cha Gilboa, na tazama, Sauli alikuwa ameegemea fumo lake; na tazama, magari na wapanda farasi wanamfuatia kwa kasi. Naye alipotazama nyuma, akaniona, akaniita. Nikajibu, Mimi hapa. Akaniambia, U nani wewe? Nikamjibu, Mimi ni Mwamaleki. Akaniambia, Tafadhali simama karibu nami, ukaniue, maana shida imenipata; kwa sababu roho yangu ingali hai ndani yangu. Basi, nikasimama karibu naye, nikamwua, kwa sababu nalijua hakika ya kuwa hawezi kupona baada ya kuanguka; kisha nikaitwaa ile taji iliyokuwa kichwani mwake, na kikuku kilichokuwa mkononi mwake, nami nimevileta hapa kwa bwana wangu. Ndipo Daudi akashika nguo zake akazirarua na kadhalika watu wote waliokuwa pamoja naye; wakaomboleza, wakalia, wakafunga hata jioni, kwa ajili ya Sauli, na kwa ajili ya Yonathani mwanawe, na kwa ajili ya watu wa BWANA na kwa ajili ya nyumba ya Israeli; kwa sababu wameanguka kwa upanga. Naye Daudi akamwambia yule kijana aliyempa habari, Watoka wapi wewe? Akajibu, Mimi ni mwana wa mgeni, Mwamaleki. Daudi akamwambia, Jinsi gani hukuogopa kuunyosha mkono wako umwangamize masihi wa BWANA? Ndipo Daudi akamwita mmoja wa vijana, akamwambia, Mwendee, ukamwangukie. Basi akampiga hata akafa. Daudi akamwambia, Damu yako na iwe juu ya kichwa chako mwenyewe; maana umejishuhudia nafsi yako ukisema, Nimemwua masihi wa BWANA.