2 Fal 20:12-21
2 Fal 20:12-21 SUV
Wakati huo Merodak-baladani mwana wa Baladani, Mfalme wa Babeli, alipeleka barua na zawadi kwa Hezekia; kwa maana alipata habari kwamba Hezekia ameugua. Hezekia akawasikiliza, akawaonyesha nyumba yote yenye vitu vyake vya thamani, fedha, na dhahabu, na manukato, na marhamu ya thamani, na nyumba yenye silaha zake, na vitu vyote vilivyoonekana katika hazina zake. Wala hapakuwa na kitu asichowaonyesha Hezekia, katika nyumba yake, wala katika ufalme wake wote. Ndipo Isaya nabii akamwendea mfalme Hezekia, akamwambia, Wasemaje watu hawa? Nao wametoka wapi kuja kwako? Hezekia akasema, Wametoka katika nchi iliyo mbali, yaani Babeli. Ndipo akasema, Wameona nini nyumbani mwako? Hezekia akajibu, Vitu vyote vilivyomo nyumbani mwangu wameviona; hapana kitu nisichowaonyesha katika hazina zangu. Isaya akamwambia Hezekia, Basi, lisikie neno la BWANA, Angalia, siku zinakuja, ambazo vitu vyote vilivyomo nyumbani mwako, na hivyo vilivyowekwa akiba na baba zako hata leo, vitachukuliwa mpaka Babeli; hakitasalia kitu, asema BWANA. Na baadhi ya wanao watakaotoka kwako, utakaowazaa, watawachukulia mbali; nao watakuwa matowashi jumbani mwake mfalme wa Babeli. Ndipo Hezekia akamwambia Isaya, Neno la BWANA ulilolinena ni jema. Tena akasema, Je! Sivyo, ikiwapo amani na kweli katika siku zangu? Basi mambo yote ya Hezekia yaliyosalia, na ushujaa wake wote, tena alivyolifanya birika na mfereji, akaleta maji ndani ya mji, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda? Hezekia akalala na baba zake; na Manase mwanawe akatawala mahali pake.