Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Fal 2:13-25

2 Fal 2:13-25 SUV

Kisha akaliokota lile vazi la Eliya lililomwangukia, akarudi, akasimama katika ukingo wa Yordani. Akalitwaa lile vazi la Eliya lililomwangukia, akayapiga maji, akasema, Yuko wapi BWANA, Mungu wa Eliya? Naye alipoyapiga maji, yakagawanyika huku na huku, Elisha akavuka. Na hao wana wa manabii, waliokuwako Yeriko wakimkabili, walipomwona, walisema, Roho ya Eliya inakaa juu ya Elisha. Wakaja kuonana naye, wakainama kifudifudi mbele yake. Wakamwambia, Angalia, wako hapa pamoja nasi watumishi wako watu hamsini walio hodari; waende, twakuomba, wamtafute bwana wako; isiwe labda roho ya BWANA imemtwaa na kumtupa juu ya mlima mmoja, au katika bonde moja. Akasema, Msiwatume. Wakamsisitiza hata akaona haya, akasema, Haya! Watumeni. Basi wakatuma watu hamsini; nao wakatafuta siku tatu, wasimwone. Wakamrudia, alipokuwa anakawia Yeriko; akawaambia, Je! Mimi sikuwaambia, Msiende? Watu wa mjini wakamwambia Elisha, Angalia, twakusihi, mahali pa mji huu ni pazuri, kama bwana wangu aonavyo; lakini maji yake hayafai, na nchi huzaa mapooza. Akasema, Nileteeni chombo kipya, mtie chumvi ndani yake. Wakamletea. Akatoka akaenda mpaka chemchemi ya maji, akatupa ile chumvi humo ndani, akasema, BWANA asema hivi, Nimeyaponya maji haya; hakutatoka huko tena kufa wala kuzaa mapooza. Hivyo yale maji yakapona hata leo, sawasawa na neno la Elisha alilolinena. Akakwea kutoka huko mpaka Betheli; naye alipokuwa akienda njiani, wakatoka vijana katika mji, wakamfanyizia mzaha, wakamwambia, Paa wewe mwenye upaa! Paa wewe mwenye upaa! Akatazama nyuma akawaona, akawalaani kwa jina la BWANA. Wakatoka dubu wawili wa kike mwituni, wakawararua vijana arobaini na wawili miongoni mwao. Akatoka huko akaenda mlima wa Karmeli, na toka huko akarudi mpaka Samaria.